2013-01-24 08:31:06

Mshikamano wa dhati na waathirika wa mafuriko Jakarta, nchini Indonesia


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumatano, tarehe 23 Januari 2013 baada ya Katekesi yake mjini Vatican, aliungana kwa njia ya sala na maelfu ya wananchi wa Indonesia ambao wamekumbwa na mafuriko na hivyo kusababisha maafa makubwa, uharibifu wa miundo mbinu na watu wengi kukosa makazi.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, anaendelea kufuatilia matukio yote haya kwa karibu na ameonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na anaendelea kuhimiza Wasamaria wema kuonesha moyo wa upendo na mshikamano na waathirika wa maafa haya, kwa kuwapatia msaada wa hali na mali.

Taarifa zinabainisha kwamba, baada ya mji mkuu wa Jakarta, Indonesia kukumbwa na mafuriko, baadaye kulifuatia tetemeko la ardhi kwenye Bahari ya Hindi, kiasi cha kuendelea kusababisha hofu na wasi wasi mkubwa. Serikali ya Indonesia imetangaza hali ya hatari, kwani hadi sasa kuna maelfu ya watu hawana mahali pa kuishi na bado wanasubiri msaada.

Mji mkuu wa Jakarta umeendelea kukumbwa na mafuriko tangu tarehe 19 Januari 2013 baada ya Bwawa kubwa mjini humo kubomoka na kusababisha vifo vya watu ishirini, kadiri ya taarifa ya Serikali, mafuriko yameendelea kutokea mara kwa mara. Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 2007 mvua kubwa iliyonyeesha mjini Jakarta, Indonesia ilisababisha watu 57 kupoteza maisha na wengine 420 kukosa mahali pa kuishi.All the contents on this site are copyrighted ©.