2013-01-24 07:42:23

Maandamano makubwa kupinga utamaduni wa kifo nchini Marekani


Kunako mwaka 1973, Serikali ya Marekani ilipitisha sheria inayo halalisha sera za utoaji mimba. Kutokana na sheria hii, wanaharakti wa kutetea zawadi ya uhai, tangu mwaka 1974, wakasimama kidete kupinga sera zinazokumbatia utamaduni wa kifo, kwa kuungwa mkono na Kanisa Katoliki nchini Marekani. RealAudioMP3

Tangu wakati huo, watetezi wa zawadi ya uhai kila mwaka ifikapo tarehe 25 Januari, wanakusanyika kufanya maandamano makubwa nchini Marekani, ili kuishinikiza Serikali kufuta sheria inayohalalisha utoaji mimba kwani inakwenda kinyume kabisa cha haki msingi za binadamu. Uhai wa mtu unapaswa kuheshimiwa tangu pale anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.

Idadi ya wadau wanaounga mkono zawadi ya uhai inaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka, kiasi kwamba, mwaka 2013 idadi ya watu wanaotarajiwa kushiriki katika maandamano haya inatarajiwa kuwa ni kubwa zaidi, wananchi wa Marekani wanapofanya kumbu kumbu ya miaka arobaini ya majonzi na simanzi kubwa kutokana na kukumbatia utamaduni wa kifo dhidi ya watoto wasiokuwa na hatia.

Maandamano haya yanatanguliwa na mkesha wa Ibada ya Misa Takatifu, unaofanyika kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili, Washington, DC na kuongozwa na Kardinali Sean Patrick O’Malley wa Jimbo kuu la Boston, Marekani.

Wakati huo huo, vijana na wakazi wanaotoka nje ya Washington DC, wanatarajiwa kufanya maandamano makubwa kuzunguka viunga vya Jiji la Washington hadi kwenye viwanja vya Congress ya Marekani, tukio ambalo litawashirikisha pia wanasiasa kadhaa kutoka Marekani; wote hawa wanalenga kutetea zawadi ya uhai, kwani ni jambo tete linalogusa zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini kwa bahati mbaya, zaidi ya miaka ishirini na mitano, sauti yao dhidi ya utamaduni wa kifo, bado inagonga kwenye masikio yaliyozibwa kwa pamba, kiasi cha kutosikia jambo lololte lile!

Utafiti uliofanywa nchini Marekani kwa Mwaka 2011 unaonesha kwamba, kuna idadi kubwa ya wananchi wanaopinga sera za utoaji mimba, kwani hii ni sehemu ya haki msingi, ambayo wanasiasa wengi wamekuwa wakiichezea kwa ajili ya mafao yao binafsi, kama wanavyofanya pia baadhi ya wahudumu wa sekta ya afya, kutokana na kuelemewa mno na uchu wa fedha. Zote hizi ni dalili na mwaliko wa kusimama kidete kulinda na kudumisha zawadi ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu.








All the contents on this site are copyrighted ©.