Viongozi wa kidini wanaendelea kuhamasisha ujenzi wa misingi ya haki, amani na utulivu
miongoni mwa Jumuiya ya Mataifa
Wakristo wanapoendelea kuombea umoja wa Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, wanapaswa
pia kusali kwa ajili ya kuombea: haki, amani na utu wa kila mtu aliyeumbwa kwa sura
na mfano wa Mungu, kama njia ya kudumisha maendeleo endelevu na ustawi wa watu wote.
Kusali kwa ajili ya kuombea amani, kuwakumbusha waamini na watu wote wenye
mapenzi mema, kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya uhai kutoka kwa Mwenyezi
Mungu, chemchemi ya haki zote msingi za binadamu.
Haya ni kati ya mawazo makuu
yaliyotolewa na Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican
kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko Geneva pamoja na Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu
mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni pamoja na viongozi wa dini na madhehebu mbali
mbali waliokusanyika hivi karibuni kwenye Kikanisa cha Kiekumene kwa ajili ya kuombea
Umoja wa Wakristo.
Siku hii iliandaliwa na Ubalozi wa Vatican mjini Geneva,
kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya kuombea amani duniani, ambayo kwa kawaida inaadhimishwa
na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe Mosi, Januari, sanjari na Siku kuu ya Bikira
Maria Mama wa Mungu "Theotokos". Tukio hili, limekuwa pia ni fursa nyingine lililowaunganisha
kwa ajili ya kusali ili kuombea Umoja wa Kanisa, kwa kuungana na Wakristo wengine
ambao tangu tarehe 18 hadi tarehe 25 Januari wanasali kwa ajili ya kuombea Umoja wa
Wakristo.
Dr. Tveit anakumbusha kwamba, mbele ya Mwenyezi Mungu, binadamu wote
wanajisikia kuwa ni Familia Moja ya watu wa Mungu, kama anavyokazia pia Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita, katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya kuombea Amani
Duniani kwa Mwaka 2013. Hii ni changamoto kwa waamini na wote wenye mapenzi mema,
kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, utu na heshima ya mwanadamu,
aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Hii ni changamoto endelevu katika ulimwengu
wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Mtakatifu Yosefu, mchumba wake
Bikira Maria na Baba mlishi wa Mtoto Yesu, anasema Dr. Tveit anaonesha jinsi alivyokuwa
mjenzi wa amani, kwa kutunza, kulinda na kuhifadhi ya maisha ya Mtoto Yesu pamoja
na Mama yake.
Ulimwengu mamboleo unawahitaji akina Mtakatifu Yosefu wengi,
ili kulinda na kuendeleza maisha ya watoto hasa wale ambao bado hawajazaliwa dhidi
ya utamaduni wa kifo unaowanyemelea siku hadi siku. Hawa ni watu ambao wanapaswa kutekeleza
mapenzi ya Mungu katika maisha yao, kwa kuendelea kuwa ni wajenzi wa haki, amani na
utulivu. Ibada hii ilihudhuriwa pia na viongozi mbali mbali wa Kidini kutoka mjini
Geneva na wawakilishi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa wanaoishi mjini hapo.