Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Vyama vya michezo, wadau na wapenda amani nchini
Kenya; kwa pamoja wamezindua kampeni inayoongozwa na kauli mbiu "Shabikia Amani na
Kura yako" inayowahamasisha wananchi nchini Kenya kushiriki kikamilifu katika mchakato
mzima wa uchaguzi, huku wakizingatia misingi ya haki, amani, umoja na mshikamano wa
kitaifa.
Lengo ni kuhakikisha kwamba, vurugu na kinzani zilizojitokeza mara
baada ya uchaguzi mkuu nchini humo katika miaka ya 1992, 1997 na ule wa mwaka 2007
uliopelekea kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kutokana na vurugu. Kampeni hii
inavihusisha vyama mbali mbali vya michezo nchini Kenya, kwani huko kuna wanachama
wengi na ujumbe unaweza kufika kwa urahisi.
Vyombo vya mawasiliano ya Jamii
vinahamasishwa pia kusaidia kuwajengea wananchi uwezo kukua na kukomaa katika masuala
ya kidemokrasia, kwa kuheshimu na kuthamini uhuru na haki msingi za binadamu. Wanasiasa
washindane kwa sera, nidhamu na uwajibikaji na wala si kwa mikuki na bunduki.
Ni
jukumu la wanasiasa kuhakikisha kwamba, wanawajengea vijana matumaini ya Kenya iliyo
bora zaidi, badala ya kuwatumbukiza vijana katika maafa yanayowaharibia mwanga wa
matumaini na maendeleo. Vita na vurugu ni sera zilizopitwa na wakati kwani zinakwamisha
mchakato wa maendeleo endelevu, kamwe vijana wasiruhusu kutumiwa na wanasiasa kwa
ajili ya malengo yao binafsi!