2013-01-23 14:43:35

Serikali ya Ufaransa kusaidia Tanzania katika huduma za maendeleo ya Jamii


Tanzania na Ufaransa zimekubaliana kuwa na mpango mwingine wa miaka mitatu ambako Ufaransa itasaidia maendeleo ya Tanzania katika nyanja mbalimbali ikiwamo ya huduma ya kijamii ikiwamo ile ya upatikanaji kwa maji safi na salama. Aidha, nchi hizo mbili zimekubaliana kuwa makubaliano hayo mapya yalenge katika kuelekeza nguvu na raslimali hizo za maendeleo katika sekta chache, mbili ama tatu, ili raslimali hizo ziweze kutumika vizuri na matokeo yake kuonekana badala ya kusambaza raslimali hizo kwa sekta na maeneo mengi.

Hayo yamefikiwa Jumanne, Januari 22, 2013 katika mazungumzo kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Ufaransa (AFD) Bwana DovZerah mjini Paris, Ufaransa ambako Rais Kikwete amemaliza ziara yake rasmi ya Kiserikali ya siku tatu.

Mara baada ya kumshukuru Bwana DovZerah kwa mchango mkubwa wa Ufaransa katika mpango wa maendeleo wa miaka mitatu kati ya 2006 na 2010, Rais Kikwete amependekeza kuanzishwa kwa mpango mpya, jambo ambalo Mkurugenzi Mkuu huyo amelikubali mara moja.

Rais Kikwete pia amependekeza kuwa raslimali katika mpango huo mpya zielekezwe katika sekta na maeneo machache, mawili ama matatu, ili raslimali hizo ziweze kutumika kwa mafanikio makubwa zaidi na matokeo yaonekane waziwazi. Chini ya mpango wa kwanza ambako Ufaransa iliipatia Tanzania kiasi cha dola za Marekani millioni 50.9 nguvu zilielekezwa katika kusaidia upatikanaji wa maji safi na salama katika miji ya Utete na Mpwapwa na katika miji midogo inayozunguka Ziwa Victoria.

Bwana Dov Zerah amemwambia Rais Kikwete: “Sisi ni washirika wenu wa maendeleo. Tuko tayari kushirikiana nanyi katika kuchangia nguvu za Serikali ya kuongoza jitihada za Watanzania kujiletea maendeleo. Nakubaliana nawe kuwa tuanzishe mpango mpya wa miaka miwili ama mitatu nauelelezwe katika maeneo machache kama unavyopendekeza.”

Kwenye siku hiyo ya pili ya ziara yake rasmi katika Ufaransa kwa mwaliko wa Rais Francois Hollande, Rais Kikwete pia amekutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Abdou Diouf, Katibu Mkuu wa Umoja wa Kimataifa wa Nchi zinazozungumza Kifaransa Duniani na Rais wa zamani wa Senegal kwenye Makao ya Umoja huo ya Maison de la Francophonie. Rais Kikwete amemweleza Rais Diouf jitihada ambazo zimekuwa zinafanywa na viongozi wa nchi wanachama wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kurudisha hali ya amani, utulivu na maelewano katika nchi ya Madagascar ambayo ni mwanachama wa Jumuia hiyo.

Mapema asubuhi, Rais Kikwete amekutana, akazungumza na kujibu maswali ya wanachama wa Watendaji Wakuuwa Makampuni ya Ufaransa (MEDEF) wakati wa mkutano wa kiamshakinywa katika mkutano uliohudhuriwa na wakubwa wa biashara na uchumi zaidi ya 50 katika Ufaransa. Kati ya wakuu wa makampuni aliokutana nao leo, makampuni 20 tayari yanaendesha shughuli zake katika Tanzania kwenye maeneo ya umeme, ujenzi, usafirishaji na biashara ya mafuta.

Aidha, Rais Kikwete amekutana na kuzungumza na Bwana Dominique Lafont, Mwenyekiti wa Kampuni ya Ballore Africa Logistics na Rais waTaasisi ya French Council for Eastern Africa na pia Bwana Phillipe Delleau, Rais wa Kampuni ya Alstom International yenye shughuli za umeme na usafiri wa reli.
All the contents on this site are copyrighted ©.