2013-01-23 11:43:11

Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania afanya mazungumzo na Rais Francois Hollande wa Ufaransa mjini Paris


Serikali ya Ufaransa imeipongeza Tanzania kwa uongozi wake katika kutafuta amani na suluhu na majawabu ya migogoro mikubwa ya kisiasa Barani Afrika katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Madagascar, Zimbabwe na Somalia. Aidha, Ufaransa imeahidi kuwa itaendelea kuunga mkono juhudi za Tanzania na wananchi wake chini ya uongozi imara wa nchi hiyo katika kujitafutia maendeleo.
Msimamo huo wa Ufaransa umeelezwa, Jumatatu, Januari 21, 2013, na Rais wa Ufaransa Mheshimiwa Francois Hollande wakati alipomkaribisha kwenye Kasri ya Uongozi wa Ufaransa ya Elysee mgeni wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa mazungumzo. Mazungumzo hayo yamehusu masuala ya uhusiano kati ya Tanzania na Ufaransa, masuala ya kanda ya Afrika na kuhusu masuala ya kimataifa.
Rais Kikwete ambaye yuko katika ziara rasmi ya siku tatu ya Kiserikali katika Ufaransa kwa mwaliko wa Rais Hollande amewasili kwenye Kasri ya Elysee kiasi cha saa tano asubuhi kamili baada ya kuwa amekaribishwa rasmi kwa gwaride rasmi kwenye Jumba la Cour d’honneur des Invalides mjini Paris.
Miongoni mwa waliohudhuria sherehe hiyo ya kukaribishwa rasmi katika Ufaransa ni pamoja na maofisa wa Serikali ya Ufaransa, mabalozi wanaoziwakilisha nchi za Afrika na nchi nyingine katika Ufaransa pamoja na maofisa wanaofuatana na Rais Kikwete kwenye ziara hiyo. Katika mazungumzo kati ya viongozi hao wawili, Rais Hollande amemwagia sifa Rais Kikwete na uongozi wa Tanzania kwa hatua na msimamo wao katika kutafuta suluhu katika migogoro kwenye ukanda wa mashariki mwa Afrika katika nchi za DRC, Madagascar, Zimbabwe na Somalia.
“Tunaipongeza sana Tanzania na uongozi wako Mheshimiwa Rais kwa jinsi mnavyohangaika kusaka amani na utulivu katika eneo la Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Kimataifa wa Eneo la Maziwa Makuu (ICGLR) katika nchi za DRC-Congo, Madagascar, Zimbabwe na kwa kiasi fulani katika Somalia,” amesema Rais Hollande na kuongeza:
“Pongezi hizi siyo za Ufaransa peke yake bali ni pongezi zinazotolewa na viongozi na mataifa mengine duniani kwa sababu mnachofanya kina manufaa ya dunia nzima.” Rais Hollande amesifia uhusiano mzuri ulioko kati ya Tanzania na Ufaransa na kuahidi kuwa Ufaransa itaendelea kuunga mkono jitihada za Tanzania na Watanzania katika kujiletea maendeleo.
Katika miaka mitano iliyopita, Tanzania imenufaika na misaada ya Ufaransa katika maeneo mbali mbali likiwemo la sekta ya maji kwa ajili ya miji midogo. Ufaransa imeipa Tanzania kiasi cha euro 50.9 kuchangia maendeleo. Msaada huo ulianza kutolewa baada ya Rais Kikwete kufanya ziara ya Ufaransa mwaka 2006 akiwa njiani kwenda Marekani. Katika kuongeza mchango wa ufaransa kwa kasi ya maendeleo ya Tanzania, Rais Hollande ameyataka makampuni zaidi ya Ufaransa kuwekeza katika uchumi wa Tanzania kuliko ilivyo sasa.
Naye Rais Kikwete amemshukuru Rais Hollande na Ufaransa kwa misaada ya maendeleo ambayo imekuwa inatolewa na nchi hiyo katika miaka mingi ya uhusiano mzuri kati ya nchi hizo mbili. Rais Kikwete pia amemshukuru na kumpongeza Rais Hollande na Ufaransa kwa uamuzi wao “thabiti” wa kuunga mkono wananchi wa Mali dhidi ya waasi wa nchi hiyo ambao walikuwa wanatishia kuiteka nchi nzima ya Afrika Magharibi.
“Hili la Mali siyo tatizo la Mali wala siyo tatizo la Afrika. Hili ni tatizo la kibinadamu na binadamu ni wamoja bila kujadili wanaishi katika eneo lipi la dunia yetu. Hivyo, tunakupongeza sana Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wako thabiti kabisa,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Tunapenda kutoa wito kwa nchi nyingine duniani kujitokeza kuungana na Wafaransa katika kusaidia watu wa Mali, kusaidia Ufaransa na kuisaidia Jumuiya ya ECOWAS katika kumaliza tatizo hilo la Mali.” Ufaransa imeingiza majeshi yake katika Mali ili kuwarudisha nyuma waasi waliokuwa wanaendelea na safari ya kuuteka mji mkuu wa nchi hiyo wa Bamako.
Mbali na kukutana na Rais Hollande, Rais Kikwete pia amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Seneti, Mheshimiwa Jean Pierre Bel; Kiongozi wa Mahedhebu ya Ismailia, H.H. The Aga Khan na Rais wa Kampuni ya Mafuta ya Total (Upstream) Bwana Yves Louis Darricarrere.
All the contents on this site are copyrighted ©.