2013-01-23 10:34:45

Padre Joakim Minja Ndelianarua, C.PP.S., kuzikwa Manyoni, Jumamosi tarehe 26 Januari 2013


Marehemu Padre Joakim Minja Ndelianarua wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania aliyefariki dunia hapo tarehe 22 Januari 2013, akiwa Parokia ya Mtakatifu Gaspar del Bufalo, Mbezi Beach, Jimbo kuu la Dar es Salaam, anatarajiwa kuzikwa kwenye Makaburi ya Wanashirika wa Damu Azizi ya Yesu, Parokia ya Kupaa Bwana Manyoni, hapo tarehe 26 Januari 2013.

Ratiba ya maziko iliyotolewa na Uongozi wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu inaonesha kwamba, Alhamisi, tarehe 24 Januari 2013, saa 10:00 kutakuwa na Ibada ya Misa Takatifu na baadaye mkesha utakaofanyika kwenye Kanisa la Mtakatifu Gaspar, Mbezi, Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Hii itakuwa ni nafasi kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam kuweza kutoa heshima zao za mwisho. Itakumbukwa kwamba, hadi mauti inamfika Padre Joakim Minja alikuwa ni Paroko Msaidizi Parokia ya Mtakatifu Gaspar, Mbezi Beach, Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Ijumaa, tarehe 25 Januari 2013, asubuhi, msafara kuelekea Manyoni, Singida kwa mazishi utaanza. Utakapofika Kisasa, Jimboni Dodoma, Makao Makuu ya Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi, watasimama kwa Ibada ya Neno la Mungu kabla ya kuendelea na safari ya kumpumzisha Marehemu Padre Joakim Minja kwenye usingizi wa amani. Itakumbukwa kwamba, hapa aliishi na kufanya utume wake kama Mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania.

Jumamosi, tarehe 26 Januari 2013, saa 4:00 asubuhi, kutafanyika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea na hatimaye maziko kwenye Makaburi ya Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, yaliyoko kwenye Nyumba Mama Manyoni, Singida. Marehemu Padre Joakim Minja Ndelianarua anakuwa ni Padre wa pili wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania kufariki dunia na kuzikwa Manyoni. Padre wa kwanza alikuwa ni Marehemu Padre Basil Ndeshingio.

Marehemu Padre Joakim Minja Ndelianarua alizaliwa kunako tarehe 4 Aprili 1966 huko Marangu, Moshi, Kilimanjaro. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kipadre huko Kibosho, Moshi, Kilimanjaro na Chuo cha Wasalvatoriani, Morogoro, alipadrishwa tarehe 7 Julai 2000, mjini Roma, kama sehemu ya kumbu kumbu ya Maadhimisho ya Jubilee kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo. Katika maisha yake aliwahi kuwa Paroko Msaidizi Parokia ya Mtakatifu Nikolaus, Mtongani, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Mkuu wa Chuo Cha Ufundi Stadi cha Mtakatifu Gaspar, Kunduchi, Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Alikuwa mchumi wa Shirika na utume wake aliutekeleza Procura, Jimbo kuu la Dar es Salaam na baadaye alichaguliwa kuwa Mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania. Hadi mauti inamfika, alikuwa ni Paroko msaidizi, Parokia ya Mtakatifu Gaspar, Mbezi Beach, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Apumzike kwa Amani. Amina.All the contents on this site are copyrighted ©.