2013-01-23 08:04:08

Miaka 40 ya Upadre si Haba! Asema Kardinali Njue!


Kardinali John Njue, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Nairobi, Jumapili, tarehe 20 Januari 2013, alimwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kutimiza miaka arobaini tangu alipopokea Daraja Takatifu la Upadre. Ibada hii ya Misa ya Shukrani ilihudhuriwa pia na baadhi ya wanadarasa wake waliosoma taalimungu pamoja mjini Roma, ambao wengi wao ni Maaskofu wa Majimbo mbali mbali duniani.

Katika mahubiri yake, Kardinali Njue alimshukuru Mungu pamoja na Familia yote ya Mungu ambayo imetembea pamoja naye katika kipindi chote hiki cha miaka 40 ambayo kwa hakika si haba! Anamshukuru kwa Maaskofu na Mapadre waliowekwa wakfu pamoja na ambao bado wako hai na wanaendelea kumtumikia Mungu na jirani zao katika Daraja Takatifu la Upadre.

Kardinali Njue anaendelea kuwataka wananchi wa Kenya kuhakikisha kwamba, wanadumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa, wakati wote wa mchakato wa uchaguzi mkuu nchini humo unaotarajiwa kufanyika hapo tarehe 4 Machi 2013. Ni wajibu wa kila mwananchi wa Kenya kuchuchumilia haki na amani, ili kufanikisha uchaguzi mkuu ambao mara nyingi umeacha kurasa chungu za misigano na kinzani miongoni mwa wananchi wa Kenya.

Kardinali Njue pia anawataka wanasiasa kuendesha kampeni za kistaarabu kwa kuheshimiana ili kutoa nafasi kwa wananchi kupima sera zitakazoweza kuwasaidia katika mchakato wa maboresho ya maisha yao kwa siku za usoni.All the contents on this site are copyrighted ©.