2013-01-23 08:29:46

Madaktari simameni kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kuzingatia: maadili, sheria, weledi na imani!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika Waraka wake wa Kichungaji Dhamana ya Afrika, "Africae Munus" anasisitizia umuhimu wa Familia ya Mungu Barani Afrika kuhakikisha kwamba, inasimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu na kamwe wasilogwe kukumbatia utamaduni wa kifo, unaofumbatwa katika sera za misaada kwa ajili ya maendeleo Barani Afrika.

Kanisa Barani Afrika linalo jukumu muhimi sana la kuwasaidia wanandoa wanaoshawishika kutoa mimba pamoja na kuendelea kuwa karibu na wote waliokwisha kumbwa na mkasa huu, ili kuwasaidia kuheshimu na kuthamini zawadi ya uhai.

Kanisa linatambua ujasiri wa serikali ambazo zimetunga sheria dhidi ya utamaduni wa kifo wakisimama kidete kuenzi utamaduni wa uhai. Waamini wanakumbushwa kwamba, wao wako ulimwenguni humu, lakini si wa ulimwengu, hivyo ni mwaliko wa kujichotea nguvu na ujasiri kutoka katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso kifo na ufufuko wa Kristo, ili kutetea zawadi ya uhai.

Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, hapo tarehe 22 Januari 2013 amezindua rasmi Chama cha Madaktari wa Kikatoliki Kenya (Kenya Catholic Doctors Association), kwa kuwataka kusimama kidete usiku na mchana kulinda na kutetea zawadi ya maisha, dhidi ya utamaduni wa kifo; daima wajitahidi kuongozwa na imani, maadili ya taaluma pamoja na weledi, ili kuwatumikia wananchi wa Kenya bila hata ya kujibakiza.

Katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Madkatari wanaalikwa kwa namna ya pekee, kuhakikisha kwamba, wanatoa huduma makini, wakisukumwa na Imani, upendo na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Kenya kwamba, Chama cha Madaktari Wakatoliki Kenya, kitakuwa mstari wa mbele kuwasaidia wanachama wake kutekeleza dhamana na wajibu wao mintarafu: sheria, kanuni, maadili na imani yao, ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kuibuliwa katika sekta ya afya na maendeleo ya sayansi ya tiba ya mwanadamu.

Kanisa linatambua na kuthamini mchango wa Madaktari wanaojitosa kimaso maso kuwahudumia ndugu zao hasa wale wanaoishi vijijini, ambako watumishi wengi wa Serikali hawapendi kwenda. Kanisa nchini Kenya, limeendelea kuwa ni mdau mkubwa wa utoaji wa huduma katika sekta ya afya, kwa kushirikiana na Serikali.

Kwa upande wao, Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Wakatoliki Kenya, Dr. Stephen Kimotho Karanja amewaambia Maaskofu Katoliki Kenya kwamba, Chama chao kimeweka kanuni msingi zinazopaswa kutekelezwa na wote wanaotaka kujiunga na Chama cha Madaktari Wakatoliki Kenya. Kati ya masharti haya ni kutojihusisha kabisa na taasisi au sera zinazokumbatia utamaduni wa kifo zinazojificha katika utoaji na vizuia mimba.

Hafla ya uzinduzi wa Chama cha Madaktari Wakatoliki Kenya ilihudhuriwa na Maaskofu kadhaa pamoja na Wafanyakazi wa Sekta ya Afya nchini Kenya.All the contents on this site are copyrighted ©.