Katiba ya Tanzania: madaraka ya Rais, Tume huru ya Uchaguzi, Udini, Muungano, Haki
ya kuishi na Umiliki wa Ardhi
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya Tanzania
mintarafu mwongozo wa uhamasishaji, leo katika makala haya wanazungumzia kuhusu madaraka
ya rais, tume huru ya uchaguzi, dhana ya kuwa na Serikali isiyokuwa na dini, muungano
na umiliki wa ardhi. Madaraka ya Rais Madaraka
ya uteuzi wa viongozi wa juu yana wigo mpana mno unaoingilia mihimili mingine ya dola
- jaji mkuu na majaji na wabunge wa kuteuliwa. Vile vile huteua mkuu wa Jeshi la polisi,
wakuu wa mikoa na wilaya nk. Pia ana mamlaka ya kusamehe wafungwa, kuvunja bunge
na baraza la mawaziri nk. Madaraka haya yanaweza kutumiwa vibaya, na pia uwajibikaji
kwa wateuliwa hao kwa wananchi unakuwa mdogo. Madaraka haya yapunguzwe na/ama yadhibitiwe.
Vigezo viwe wazi na uamuzi ufikiwe kwa njia shirikishi. Tume huru ya uchaguzi na
Tume nyinginezo Kwa sababu inaundwa kwa njia ya uteuzi bila vigezo kuwekwa wazi,
wananchi wengi wamekosa imani nayo, na malalamiko yamekuwa mengi. Uundwaji wa Tume
zetu ufanyike kwa uwazi na iliyo shirikishi. Dhana ya kuwa Serikali haina dini
(Secularity of the State) Msingi huu ndio nguzo ya umoja na amani katika nchi yetu.
Ifafanuliwe na kusimamiwa kikatiba ikiwa ni pamoja na kuweka mipaka katika uhuru wa
kuabudu kwa kuwa tumeshaona unatumika vibaya kama vile kuleta mgawanyiko na mtikisiko
katika familia, kufanya mihadhara ya kukashifu dini nyingine, kuharibu mali za wengine
na kusababisha uvunjifu wa amani. Vile vile msukumo wa kuanzisha mahakama ya kadhi
ndani ya mfumo wa mahakama za nchi siyo haki kwa hiyo isiwemo katika Katiba kwa kuwa
ni mambo ya kidini na huenda ni njia ya kuifikisha nchi yetu katika kukiuka dhana
ya kuwa serikali yetu haina dini. Muungano Kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya
Zanzibar, Katiba ya Muungano imevunjwa, wakati huo huo msukumo wa watu kutaka Muungano
uangaliwe upya una hoja zenye nguvu. Tutoe maoni yetu tukizingatia sababu za waasisi
wa muungano, na pia faida na hasara za muungano kwa wakati huu. Mapendekezo ya kutambua
Tanganyika kama nchi yametambuliwa na Katiba ya sasa ya Zanzibar, kwa hiyo wazo la
kuwa na Muungano wenye Serikali tatu ni hoja ambayo tunaweza kutolea maoni yetu. Haki
ya kuishi Kwetu sisi Wakatoliki ni jambo la kupigania kwa nguvu zote Katiba iweze
kulinda uhai tangu kutungwa mimba. Vile vile tunaweza kutoa maoni yetu juu ya adhabu
ya kifo. Hapa tuna wajibu wa pekee kabisa kutoka imani yetu inayotufundisha kwamba
mwenye mamlaka ya kutoa uhai na kuutwaa ni Mungu Mwenyewe. Umiliki ardhi Haki
ya watu wa Tanzania Visiwani kumiliki ardhi ya Bara ifutwe kama ilivyo kwa watu
kutoka Tanzania Bara kutoweza kumiliki ardhi huko Visiwani.