2013-01-22 09:59:53

Zaidi ya watu millioni 197 hawana fursa za ajira duniani


Shirika la Kazi Duniani, ILO, katika taarifa ya mwenendo wa ajira duniani kwa kipindi cha miaka mitano inaonesha kwamba, watu wengi wanaendelea kukabiliana na ukosefu wa fursa za ajira, kwa kipindi cha miaka mitano sasa kutokana na athari za myumo wa uchumi kimataifa.

Katika kipindi cha Mwaka 2012, idadi ya watu wasiokuwa na ajira duniani imeongezeka kwa asilimia 5.9%, ambao ni watu millioni 4.2. Shirika la Kazi Duniani linasema, kwa sasa kuna zaidi ya watu millioni 197 wasiokuwa na ajira. Waathirika wakubwa ni wananchi wanaotoka katika Nchi zilizoendelea zaidi duniani. Kuna dalili za kukua kwa uchumi kwa nchi zilizoko Asia na Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Hayo yamebainishwa na Bwana Guy Ryder, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kazi Duniani. Sera mbaya kuhusu soko la ajira zimepelekea watu wengi kukosa fursa za ajira, changamoto ya kuwekeza zaidi kwa vijana. Hata hivyo ukuaji wa uchumi kimataifa bado unaendelea kusua sua kiasi kwamba, haitakuwa rahisi kwa kipindi cha muda mfupi Jumuiya ya Kimataifa kuweza kutoa ajira kwa watu millioni 210 wanaotafuta ajira.

Kuna vijana zaidi ya millioni 74 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24 hawana fursa ya ajira duniani. Wote hawa ni sawa na asilimia 12.6%.







All the contents on this site are copyrighted ©.