2013-01-22 07:38:38

Maoni ya Katiba Mpya ya Tanzania: uteuzi wa viongozi, huduma bora za kijamii, haki za binadamu, ukubwa Serikali na Bunge; mgawanyo wa madaraka


Jaji Joseph Sinde Warioba, Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba hivi karibuni amenukuliwa akisema kwamba, Mwezi Februari, 2013, Tume itaanza kuchambua maoni na baadaye, kuandika Rasimu ya Katiba Mpya ya Tanzania inayotarajiwa kuwa imekamilika mwezi Juni, 2013. Hatua itakayofuatwa ni kupelekwa kwa Mabaraza ya Kikatiba na kwamba, Tanzania inatarajia kupata Katiba Mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa Mwaka 2015. RealAudioMP3
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linaendelea kuhamasisha waamini na watanzania wenye mapenzi mema kuangalia changamoto zifuatazo ili ziweze kufanyiwa kazi wakati wa kuandika Katiba Mpya: Uteuzi wa viongozi; huduma bora za kijamii na haki za binadamu; ukubwa wa Serikali na Bunge; Mgawanyo wa madaraka pamoja na Madaraka ya Rais.

Kwa mujibu wa Katiba ya sasa Rais ana madaraka makubwa mno. Vigezo vinavyotumika haviko wazi na mara kadhaa imeonekana wanashindwa kutimiza majukumu yao kwa sababu wamepewa kazi ambayo hawana uwezo nayo. Hata inapodhihirika hivyo bado imekuwa vigumu mno kuwaondoa madarakani.

Vigezo vya kidini na kinasaba pia vimekuwa vikilalamikiwa kuwa vinatumika. Kwa mteuliwa husukumwa kutumikia matakwa ya aliyemteua badala ya kuwa mtumishi wa wananchi. Katiba ijibu changamoto hii kwa kuweka sifa na vigezo kadiri ya mahitaji ya nafasi husika na pia njia ya kuwajibisha. Uteuzi usibaki kwa mtu mmoja bali ufanyike kwa njia shirikishi kupitia Tume huru.

Huduma bora za jamii na haki za binadamu

Haki hizi ni pamoja na huduma za afya, elimu, maji, miundombinu nk. Haki hizi zaweza kulenga mtu mmoja mmoja , makundi maalum kama vile walemavu, wazee na maskini ama jamii nzima. Kutimiza haki hizi serikali na wananchi wote wanawajibika kila mmoja kwa nafasi na kiwango chake. Haki hizi ziainishwe katika Katiba na Katiba ihakikishe zinatekelezeka kisheria.

Ukubwa wa Serikali

Tunaweza kuwa na serikali ndogo ambayo inafanya kazi kwa ufanisi. Hapa tuangalie idadi ya wizara na mawaziri, na hata mgawanyo wa mikoa na wilaya. Tunaweza kupunguza gharama za uendeshaji kwa kupunguza maeneo haya na hivyo kuweza kuongeza fungu katika bajeti ya maendeleo na mahitaji mengine muhimu ambayo tunakwama kuyagharamia. Katiba iainishe hayo isiwe ni matakwa ya kila awamu ya uongozi.

Ukubwa wa Bunge

Kwa nia hiyo hiyo ya kupunguza gharama inafaa kuangalia upya nafasi za ubunge wa kuteuliwa na wa viti maalum. Kimsingi mbunge ni mwakilishi wa wananchi ambao wanaweza kumwajibisha, na aelewe anabeba dhamana kubwa na anapaswa kuchapa kazi kwa umahiri na weledi.

Mgawanyo wa madaraka

Hii ni kanuni msingi ya demokrasia na utawala bora. Kibinadamu ni jambo msingi kwa sababu inatoa nafasi ya kusahihishana na hivyo kukabiliana na madhaifu ya kimaumbile. Mihimili mikuu ya dola – Bunge, Mahakama na Serikali yapasa vifanye kazi kwa uwajibikaji na kuwajibishana na sio katika mwingiliano. Kwa hali ilivyo sasa tunaona kuna mwingiliano mkubwa na hata tunaona serikali hukimbilia mahakama (isiyo huru) kama kichaka kuficha udhaifu katika utendaji wa majukumu yake, hasa kukwepa kutimiza haki za watu.

Kwa namna hii utawala wa sheria unakuwa mgumu kudhihirika. Katiba iimarishe kanuni hii kwa kutoruhusu wabunge kuwa mawaziri, majaji kutoteuliwa na Rais nk. Wananchi wapewe uwezo wa kudhibiti mihimili ya dola kwa kuweka Mahakama ya Katiba kupeleka mashauri yao pale wanapoona kuna ukiukwaji wa Katiba katika utekelezaji wa majukumu yao.

Madaraka ya Rais

Madaraka ya uteuzi wa viongozi wa juu yana wigo mpana mno unaoingilia mihimili mingine ya dola - jaji mkuu na majaji na wabunge wa kuteuliwa. Vile vile huteua Mkuu wa Jeshi la Polisi, Wakuu wa mikoa na wilaya nk. Pia ana mamlaka ya kusamehe wafungwa, kuvunja Bunge na Baraza la Mawaziri nk. Madaraka haya yanaweza kutumiwa vibaya, na pia uwajibikaji kwa wateuliwa hao kwa wananchi unakuwa mdogo.

Madaraka haya yapunguzwe na/ama yadhibitiwe. Vigezo viwe wazi na uamuzi ufikiwe kwa njia shirikishi.








All the contents on this site are copyrighted ©.