Hotuba ya Rais Obama wakati wa kula kiapo cha Utii, Awamu ya Pili kama Rais wa Marekani
Rais Barack Hussein Obama wa Marekani, tarehe 21 Januari 2013 ameanza awamu ya pili
ya uongozi wake kama Rais kwa kula kiapo cha kuilinda na kuitetea Katiba ya nchi,
kama kielelezo makini cha demokrasia na Umoja wa Kitaifa, unaowafanya wote wajisikie
kuwa ni raia wa Marekani.
Kila mwanadamu
ana haki ya maisha, uhuru pamoja na kushiriki katika mchakato utakaompatia furaha
ya kweli; mambo ambayo daima yamekumbana na kinzani, kiasi hata cha kupelekea uwagaji
wa damu, ili kusimamia misingi ya haki, usawa na uhuru.
Rais Obama katika hotuba
yake kwa umati wa watu uliofurika kwenye Viwanja vya Ikulu ya Marekani, amehimiza
umuhimu wa kuwekeza katika sekta ya elimu, ili kuweza kukabiliana na ushindani wa
haki na fursa sawa unaojitokeza katika sekta ya uchumi na soko huria; kwa kuzingatia
kanuni, sheria na maadili. Wananchi wanapaswa kuwajibika pamoja na kufanya kazi kwa
juhudi na maarifa, kama kielelezo cha utambulisho wao.
Katika mabadiliko yanayoendelea
kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kuna
haja ya kujenga na kuimarisha mshikamano wa kimataifa, ili kukabiliana na changamoto
zinazoibuliwa katika masuala ya kidemokrasia, elimu, uchumi na fursa za ajira. Marekani
ambayo ni taifa lenye nguvu kiuchumi, lakini katika miaka ya hivi karibuni, limetikiswa
na athari za myumbo wa uchumi kimataifa.
Taifa halina budi kuwekeza katika
nguvu ya vijana na kuwasaidia watu wengi zaidi kuboresha hali ya maisha yao ili kupata
maendeleo ya kweli ambayo ni matunda ya kazi na malipo halali na kwamba, kila mtu
anayo haki ya kuondokana na umaskini wa kipato mintarafu misingi ya uhuru na usawa
mbele ya Mungu na Wanadamu. Ili kufikia malengo haya kuna haja ya kuendelea pia kuwekeza
katika maendeleo ya teknolojia, ukusanyaji makini wa kodi, maboresho katika mfumo
wa elimu na kuwajengea wananchi uwezo wa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.
Rais
Obama katika hotuba yake iliyokuwa inafuatiliwa na mamillioni ya watu kutoka sehemu
mbali mbali za dunia, alikazia umuhimu wa kulinda usalam, kudumisha utu wa mwanadamu,
usawa na uhuru kwa watu wengi zaidi na wala si kwa ajili ya kikundi cha watu wachache
ndani ya Jamii, ili kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoweza kujitokeza. Hii
ndiyo mantiki inayofumbatwa katika maboresho katika sekta ya afya na hifadhi za kijamii
zinazowaimarisha kama Jamii ya wananchi wa Marekani.
Wanaharakati wa kulinda
na kutunza mazingira wamempongeza Rais Obama kwa kukazia umuhimu wa kulinda na kutunza
mazingira pamoja na kuwajibika barabara kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia
nchi, kwa sasa na kwa ajili ya kizazi kijacho. Athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoambatana
na: mafuriko, ukame, tufani na majanga ya moto ni changamoto ya kuwekeza katika nishati
na teknolojia rafiki kwa ajili ya maendeleo endelevu, kwa kuzingatia fursa za ajira
na ukuaji wa uchumi, kwa kutambua kwamba, kila mtu anahamasishwa kulinda na kutunza
mazingira kama sehemu ya kazi ya uumbaji.
Rais Obama anabainisha kwamba, usalama
na amani ya kudumu vina gharama yake na kwamba, umefika wakati kwa wananchi wa Marekani
kuwa macho na wote wanaotaka kuwashambulia; lakini wanapaswa pia kutafuta amani na
kujenga urafiki. Amerika itaendelea kuwalinda watu wake kwa njia ya silaha na utawala
wa sheria; itatafuta suluhu kwa njia ya amani na kushikamana na mataifa mengine katika
kudumisha misingi ya haki na amani; demokrasia na uhuru.
Nchi ya Marekani itaendelea
kuwa ni chemchemi ya matumaini kwa maskini, wagonjwa na wote wanaosukumizwa pembezoni
mwa Jamii, ili kujenga na kudumisha amani inayojikita katika misingi ya kuvumiliana,
fursa sawa, utu na heshima ya mwanadamu na usawa. Hii ni safari ndefu inayopania kutoa
haki na usawa kwa kuzingatia utawala wa sheria, sera makini kwa wahamiaji ili kushiriki
katika maendeleo na ustawi wa Amerika pamoja na kuhakikisha usalama wa watoto wao
dhidi ya mashambulizi. Kila mtu anayo haki ya kufurahia maisha.
Rais Obama
anasema, amekula kiapo kwa Mungu na kwa ajili ya nchi yake, changamoto ya kuhakikisha
kwamba, kweli anakuwa mwaminifu kwa Katiba wakati wote anapokuwa madarakani. Kama
raia, kwa pamoja wanapaswa kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha
ya kijamii.