2013-01-21 08:01:32

Uwekezaji katika sekta ya kilimo upewe msukumo wa pekee ili kukabiliana na baa la njaa na umaskini wa kipato!


Josè Graziano da Silva Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO pamoja na Ilse Aigner, Waziri wa Chakula, na Kilimo na Usalama wa Walaji kutoka Ujerumani, kwa mara nyingine tena, wameendelea kuhimiza Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza zaidi katika sekta ya kilimo ili kupambana kufa na kupona na baa la njaa linaloendelea kutishia maisha ya mamillioni ya watu duniani, sanjari na kuhakikisha usalama wa chakula kutokana na ongezeko la watu duniani.

Taarifa za FAO zinaonesha kwamba, uwekezaji katika sekta ya kilimo bado uko chini sana, ikilinganishwa na mahitaji ya chakula na mazao ya biashara kwa sasa katika soko la kimataifa. Wakulima ni wadau wakuu katika mchakato wa kuhakikisha usalama wa chakula na ukuaji wa uchumi katika nchi zinazoendelea duniani.

Serikali ya Ujerumani inatumia zaidi ya Euro million 700 kila mwaka kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa chakula na maendeleo endelevu vijijini katika nchi changa zaidi duniani. Lengo ni kuongeza tija na uzalishaji kutoka kwa wakulima wadogo wadogo vijijini. Fedha hii inagharimia mafunzo ya kilimo vijijini.

Bwana Da Silva anasema kwamba, kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wan chi nyingi na wakulima wadogo wadogo ni wadau wakuu katika mapambano dhidi ya baa la njaa na umaskini wa kipato miongoni mwa mamillioni ya watu wanaoishi vijijini. Ni jukumu la Serikali husika kwa kusaidiana na Jumuiya ya Kimataifa kuwajengea wakulima uwezo wa kuwekeza zaidi katika sekta ya kilimo ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, ili kukuza pato la wakulima, kutunza mazingira na kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira.

FAO inaonesha kwamba, kuna jumla ya watu million 870 wanaoendelea kutopea katika lindi la umaskini wa kipato na kuna idadi kubwa ya watu wanaokabiliwa na baa la njaa kila mwaka na kwamba, wengi wao ni wale wanaoishi vijijini. Wakulima vijijini wanapaswa kuwa ni walengwa wakuu katika sera na mikakati ya uwekezaji katika sekta ya kilimo. Wasaidiwe kuondokana na vizingiti vinavyokwamisha maendeleo ya sekta ya kilimo.

Ili kufanikisha malengo haya, kuna haja ya kuwa na utawala bora, kupewa motisha; kuwa na uhakika wa miundo mbinu na soko; huduma bora za kijamii na maboresho katika njia za mawasiliano. Ni jukumu la Serikali husika kuhakikisha kwamba, mazingira haya yanapatikana kwa wakulima ili waweze kuzalisha chakula cha kutosha ili kuondokana na baa la njaa pamoja na kuwa na uhakika wa usalama wa chakula kwa sasa na kwa siku zijazo.
All the contents on this site are copyrighted ©.