2013-01-21 15:30:42

Usalama wa Wakristu Mali mashakani- Askofu Sengue


Kanisa Katoliki nchini Mali, limeonyesha kushakia usalama wa Wakatoliki na Wakristu kwa ujumla, kwa kadri ghasia za mapigano zinavyoendelezwa na Wababe wa Kiislamu wenye silaha, walioasi serikali na kutwaa baadhi ya maeneo ya nchi hiyo, hasa eneo la Kaskazini mwa Mali.

Askofu Augustino Traore Sengue, ambaye Jimbo lake liko katika eneo lililotekwa nyara na waasi wa Kiislamu wasiovumilia wengine, anasema , ingawa mpaka sasa hakuna mashambulizi ya moja kwa moja katika makanisa, Wakristu wana woga mkubwa wa kwenda kusali katika makanisa au kuadhimisha ibada zao kwa uhuru na kama wanavyopaswa.

Hivyo wengi wamefichama majumbani mwao, wakiwa wamegubikwa na woga mkubwa wa kutoka nje. Hawana la kufanya bali kusubiri hadi hapo wenye mamlaka ya kitawala,watakapoweza kupata suluhu ya kusitisha ukatili huo. Wakristu hao hawana uhakika na kitakacho watokea wao wenyewe au kwa majengo ya Makanisa iwapo waasi watatwaa utawala katika eneo la Kaskazini mwa Mali.

Askofu Augostino ameonyesha wasiwasi wa kushambuliwa kwa makanisa na wababe hao, ingawa kwa wakati huu anasema, bado kuna mahusiano mazuri kati ya Wakristu na waislamu wenye kuwa na kiasi. Na kwamba, wote wenye mapenzi mema bado wanaonyesha kuwajibika na udumishaji wa umoja na mshikamano , wengi wao wakitamani ghasia za mapigano yanayoendelea zisitishwe mara moja.

Habari inasema, kwa wakati huu , zaidi ya raia 200,000 wa Mali wamehama maeneo yao na kuelekea maeneo ya Kusini mwa Mali ambako kuna usalama zaidi . Na watu wengine wamevuka mpaka na kuingia katika mataifa ya Niger, Nigeria, Burkina Faso , Morocco na Algeria.

Kanisa Katoliki Mali , lina Majimbo sita yanayohudumia Wakatoliki wapatao asilimia mbili ya raia wote wa Mali wapatao millioni 15.8, ambayo wengi wao ni Waislamu .

Maasi yanayoendeshwa katika eneo la Kaskazini, yalizuka tangu March mwaka jana 2012, ambako waasi hao wanaodai Sharia za Kiislamu zitawale, wamekwisha fanya umwagaji wa damu mwingi na uharibifu mkubwa wa mali na kumbukumbu katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa historia.

Katikati ya mwezi huu Januari, Askofu Mkuu Jean Zerbo wa Bamako , aliomba ujia wa usalama utolewe, kwa ajili ya upelekaji wa misaada ya kibinadamu kwa umma unaoteswa na ghasia hizo, watu wasiokuwa na hatia hasa wanawake na watoto .
All the contents on this site are copyrighted ©.