2013-01-21 07:52:55

Serikali ya Kenya yaombwa kuchunguza kwa kina vurugu za mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji Mkoa wa Bonde la Mto Tana


Askofu mkuu Zacchaeus Okoth, Mwenyekiti wa Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, hivi karibuni ameongoza ujumbe wa viongozi watano kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya ili kutembelea Mkoa wa Bonde la Mto Tana ambao hivi karibuni umekuwa ni uwanja wa fujo na mauaji ya kinyama kutokana na kinzani za kikabila pamoja na kugombea ardhi kwa wakulima na malisho kwa wafugaji.

Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Kenya unaitaka Serikali ya Kenya kuhakikisha kwamba, inatumia vyema vikosi vya ulinzi na usalama ili kusitisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia yanayoendelea kujitokeza nchini Kenya sanjari na uharibifu wa mali ya raia. Wanaiomba Serikali kuangalia uhusiano uliopo kati ya rasilimali na kinzani za kikabila na kwamba, wahusika wakamatwe na kufikishwa mbele ya sheria, ili iweze kuchukua mkondo wake.

Wananchi wamechoshwa kusikia vurugu na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia kwa kisingizio cha kugombania malisho ya wanyama. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, limeiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuunda tume inayojitegemea ili kufanya uchunguzi wa kina dhidi ya Jeshi la Polisi kama linawajibika kwa kutotekeleza wajibu wake kuzuia mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Umefika wakati kwa Serikali kuangalia sera ya umiliki wa ardhi ambayo imekuwa kwa muda mrefu chanzo cha kinzani na misigano ya kijamii nchini Kenya.

Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Kenya, linawaalika wananchi wanaoishi katika Mkoa wa Bonde la Mto Tana, kuondokana na chuki na uhasama, kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama Wananchi wa Kenya, daima wakijikita kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa.

Baada ya vurugu na kinzani zote hizi, kuna haja sasa ya kujenga utamaduni wa msamaha na upatanisho, ili amani ya kweli iweze kurejea tena miongoni mwa wananchi hawa, vinginevyo, mzunguko wa machafuko utaendelea kuwa ni chanzo cha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia na kikwazo cha maendeleo endelevu, kwani hakuna maendeleo mahali ambapo vita inaendelea kurindima kila siku.








All the contents on this site are copyrighted ©.