2013-01-21 08:35:54

Onesheni mshikamano wa dhati na watu wenye ulemavu kwa kuwawezesha kiuchumi ili wajitegemee!


Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema, suala la uchangiaji wa VICOBA kwa ajili ya watu wenye ulemavu linahitaji kupangiwa mkakati maalum ili zipatikane fedha za kutosha kuwapa mitaji nao pia wajitegemee. Amesema yuko tayari kukaa na Mkurugenzi Mtendaji wa IPP, Bw. Reginald Mengi ili wabungue bongo ya jinsi ya kutunisha mfuko wa VICOBA kwa ajili ya watu wenye ulemavu.

Ametoa ahadi hiyo Jumapili, Januari 20, 2013 wakati akizungumza na watu wenye ulemavu wa mkoa wa Dar es Salaam katika hafla yao ya chakula cha mchana ya kuukaribisha mwaka mpya 2013 iliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam. Hafla hiyo iliandaliwa na Bw. Mengi.

“Bwana Mengi amewasha moto mzuri kwa kuwachangia hawa watu sh. milioni 100. Nimeambiwa kuwa walianza kwa kujichangisha sh. milioni 17. Najua nami nawajibika kuwachangia lakini itabidi nikae naye tuone jinsi huduma hii inavyoweza kusambaa na kuwafikia Watanzania wengi zaidi,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema ili uwe mpango endelevu, wabuni mpango utakaowajumuisha Watanzania wengi zaidi, wakiwemo wanasiasa, viongozi wa dini na wengine wengi. “Nia yetu ni kila mwenye nacho achangie ili kuwasadia wenzetu wawe na miradi ya kujikimu kimaisha kupitia mikopo ya VICOBA,” alisema.

Akijibu risala ya watu wenye ulemavu iliyosomwa na Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Bi. Lupi Maswanya ambayo ilikumbushia ombi la kupatiwa Ofisi ya kudumu, Waziri Mkuu alisema ahadi yao bado anaikumbuka, hajaisahai ila bado naifanyia kazi.

Katika risala yao, watu wenye ulemavu pia waliiomba Serikali iharakishe kutoa kanuni za Sheria Na. 9 ya mwaka 2010 ya Haki za Watu wenye Ulemavu ili kuharakisha muundo wa Baraza la walemavu na kamati zake.

“Pia tunaiomba Serikali itohoe kwa lugha nyepesi na kuitangaza sheria hiyo katika vyombo mbalimbali ikiwemo kuiweka kwenye maandishi ya nukta nundu kwa ajili ya watu wenye uoni hafifu,” ilisema sehemu ya risala yao.

Pia walimuomba Rais Jakaya Kikwete amteue Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Taifa la Watu wenye Ulemavu ili kuharakisha uundwaji wa Baraza na Kamati zake kwa mujibu wa sheria hiyo.

Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu kuongea na hadhara hiyo, Bw. Mengi aliiomba Serikali iangalie uwezekano wa kukabili tatizo la dawa za kulevya kwa namna ya pekee kwani linachangia kwa kiasi kikubwa tatizo la watu wenye matatizo ya akili nchini. “Hawa nao wanageuka kuwa watu wenye ulemavu wa akili,” alisema.

Naye muasisi wa VICOBA nchini, Bi. Devotha Likokola alisema kikundi cha watu wenye ulemavu kimefikisha wanachama 150 lakini kinakabiliwa na changamoto ya waombaji wengi wenye ulemavu hasa kutoka mikoani.

“Mfuko huu waliuanzisha wao wenyewe, na kuamua kukopeshana ili wafanye biashara. Bw. Mengi akawaongezea sh. milioni 100. Wamesema wakiwezeshwa wanahitaji miaka mitano tu nao wataanza kufadhili watu wengine,” alisema Bi. Likokola.
All the contents on this site are copyrighted ©.