2013-01-21 09:34:51

Katiba Mpya ya Tanzania ijibu changamoto kuhusu: rushwa na ufisadi; mgawanyo wa rasilimali za nchi; uwajibikaji na vyombo vya kusimamia na kutoa haki!


Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika kuhamasisha utoaji wa maoni katika mchakato wa kuandika Katiba mpya linabainisha kwamba, nia ya maoni haya ni kusaidia waamini wetu kutafakari na kupata uelewa na hivyo kuweza kutoa maoni makini kwa faida ya jamii yetu na Taifa letu. Maoni haya yamejikita hasa katika changamoto zifuatayo: RealAudioMP3
    Rushwa na ufisadi

Tukumbuke Rushwa nia adui wa haki sitapokea wala kutoa rushwa. Hadi sasa miaka hamsini ya uhuru wetu tunaona rushwa inazidi kukua na kuenea. Na imejikita pia hadi kwenye vyombo vikuu vya utawala (Polisi, Mahakama, Serikali na Bunge) na inaelekea vigumu kuidhibiti. Tatizo hili kongwe linahusu jamii nzima – kushiriki kwa kutoa au kupokea ama kufumbia macho. Matokeo yake rushwa na ufisadi imetuathiri sote kama wananchi na kama Taifa. Tutoe maoni yetu kuonyesha ni namna gani tatizo hili linaweza kutatuliwa kisheria na kijamii. Tutazame upya jinsi ya kuimarisha vipengele vya kudhibiti ukiukwaji wa maadili kwa viongozi na pia kuona kama TAKUKURU kama ni chombo huru na chenye meno kisheria.

    Mgawanyo wa mali na rasilimali za nchi

Hizi ni pamoja na ardhi, madini, mafuta/gesi, misitu, mbuga za wanyama, bahari, maziwa na mito, bila kusahau mfuko wa taifa (hazina). Utajiri huu ni majaliwa ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi wa Watanzania wote kwa vizazi na vizazi. Hali ilivyo sasa ni tofauti na azma hiyo. Wachache wamejilimbikizia na wengi wanaendelea kuishi maisha duni, kumekuwa na mgawanyo wa matabaka ya wenye nacho na wasio nacho. Kijumla wanyonge wametupwa pembeni katika maendeleo ya kiuchumi. Wawekezaji kutoka nje wanapewa kipaumbele dhidi ya wananchi kwa njia ya mikataba kusainiwa katika usiri mkubwa. Mwelekeo huu unahatarisha amani na hadi sasa kumekuwa na matukio mengi ya uvunjifu wa amani katika jitihada za wananchi kujaribu kutetea maslahi yao. Katiba iweke namna ya kuhakikisha wananchi wote wanashiriki katika kutumia rasilimali zetu kwa maendeleo ya wote na kuzitunza kwa ajili ya vizazi vijavyo.

    Uwajibikaji : raia na viongozi kwa ngazi na makundi yote

Kadiri siku zinavyokwenda moyo wa uwajibikaji unaendelea kufifia tangu ngazi ya familia. Jamii inakosa kushikamana katika kujiletea maendeleo na ustawi na hata huharibu miundombinu iliyowekwa kwa ajili yao. Viongozi wanakiuka maadili na kuliingizia Taifa hasara kubwa na bado hakuna kuwajibika ama kuwajibishwa. Kwa hiyo tunaona mfumo wa uwajibikaji kijumla sio mzuri. Katiba iweke taratibu wa kung’olewa madarakani kwa sababu ya kutowajibika, iimarishe njia za kudhibiti madaraka (checks and balance), bunge liwe kweli mwakilishi wa wananchi na mijadala yake iongozwe katika hali ya kuruhusu maoni mbadala na kuyaheshimu. Raia wasibaki katika kulalamika tu, bali waonyeshe mamlaka yao na nguvu yao katika suala zima la uwajibilkaji.

    Vyombo vya kusimamia na kutoa haki

Hapa tulenge mahakama na polisi. Vyombo hivi vimeshindwa kufikia matarajio ya wananchi. Zaidi vimekuwa upande wa wenye fedha na madaraka na kwa wananchi wa kawaida na hasa wanyonge imekuwa ni vigumu mno kupata haki zao. Kwa upande mwingine wananchi nao wanashiriki kuvifanya vyombo hivi vishindwe kutimiza majukumu ya uwepo wake mfano kwa njia ya kushiriki rushwa, wakati mwingine ikiambatana na kubambikiza kesi, polisi kutesa na kudhalilisha, kuchelewesha mno kesi na pengine hukumu ikitoka kuonyesha kuwa mhabusu hakuwa na kosa nk. Katiba iwezeshe vyombo hivi kuwa huru na hivyo kutenda haki sawa kwa wote badala ya kuegemea upande fulani.
All the contents on this site are copyrighted ©.