2013-01-21 07:42:58

Kanisa nchini Pwani ya Pembe linamkumbuka Hayati Askofu mkuu Ambrose Madtha


Baraza la Maaskofu Katoliki Pwani ya Pembe, limehitimisha mkutano wake wa Mwaka, Jumapili tarehe 20 Januari, uliokuwa umefunguliwa hapo tarehe 15 Januari 2013, kwa kumbu kumbu ya kifo cha Askofu mkuu Ambrose Madtha, aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Pwani ya Pembe.

Askofu mkuu Madtha alifariki kwa ajari ya gari hapo tarehe 8 Desemba 2012 alipokuwa anatoka katika maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili. Mkutano huu umekuwa ni kipindi cha neema na baraka pamoja na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa Maaskofu Katoliki wa Pwani ya Pembe.

Maaskofu hao pamoja na mambo mengine, wamejadili hali ya maisha na utume wa Kanisa na Jamii kwa ujumla. Kanisa nchini Pwani ya Pembe ni hai na linaendelea kusonga mbele kwa imani na matumaini makubwa, licha ya changamoto na kinzani mbali mbali zinazoendelea kujitokeza. Maaskofu wanaendelea kuhimiza waamini na wananchi wa Pwani ya Pembe, kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa, ili kujipatia maendeleo endelevu.
All the contents on this site are copyrighted ©.