2013-01-21 08:56:36

Boresheni imani yenu kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya Sala ya Kanisa yenye utajiri mkubwa kutoka katika Zaburi


Mama Kanisa anawaalika watoto wake katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, kuendelea kuboresha imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya Sala na Tafakari ya Neno la Mungu; Maisha ya Kisakramenti na Matendo ya huruma, kama kikolezo cha imani tendaji.

Leo katika makala hii, tunaye Mheshimiwa Padre Stephano Kaombe, Gombera wa Seminari Ndogo ya Visiga, Jimbo kuu la Dar es Salaam, anayetushirikisha tafakari ya Zaburi ya 96. Ikumbukwe kwamba, Sala za Kanisa ni kwa ajili ya Wakristo wote, kumbe kuna haja ya kujenga utamaduni wa kusali Sala za Kanisa. Basi huu uwe ni mkakati maalum katika maadhimisho ya Mwaka wa Kanisa.

Dominika 2 Mwaka C.
ZABURI 96

Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
mwimbieni Bwana, nchi yote.
Mwimbieni Bwana, libarikini jina lake,
tangazeni wokovu wake siku kwa siku.
Wahubirini mataifa habari za utukufu wake,
na watu wote habari ya maajabu yake.

Kwa kuwa Bwana ni mkuu mwenye kusifiwa sana,
na wa kuhofiwa kuliko miungu yote.
Maana miungu yote ya watu si kitu,
lakini Bwana ndiye aliyezifanya mbingu.
Heshima na adhama ziko mbele zake,
nguvu na uzuri zimo katika patakatifu pake.

Mpeni Bwana, enyi jamaa za watu,
mpeni Bwana utukufu na nguvu,
mpeni Bwana utukufu wa jina lake.
Leteni sadaka mkaziingie nyua zake,
mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu wake;
tetemekeni mbele zake, nchi yote.

Semeni katika mataifa, “Bwana ametamalaki!”
Naama, ulimwengu umethibitika usitikisike,
atawahukumu watu kwa adili.

Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie,
bahari na ivume na vyote viijazavyo,
Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo,
ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha;
mbele za Bwana, kwa maana anakuja,
kwa maana anakuja aihukumu nchi.
Atahukumu ulimwengu kwa haki,
na mataifa kwa uaminifu wake.

Zaburi hii inasadikiwa ilitungwa wakati Waisraeli walipokuwa wanajiandaa kurudi tena katika nchi yao ya ahadi, toka Uhamishoni Babeli, ndiyo mazingira yake. Walikuwa wamejaa matumaini na furaha kuu, kutokana na wema Mungu aliowatendea wa kuwapa nafasi nyingie tena kurejea kwao. Hakuna jambo lililokuwa la thamani kama kwao kumtolea Mungu sadaka ya wimbo wa sifa.

Iwe ni mwanzo wa mwaka, mwezi, siku mpya tunapoifungua mioyo yetu au tunapoanza Uinjilishaji mpya; tujiunge na mzaburi kumwimbia Mungu wimbo mpya wa sifa. Upya si katika kuanza mwaka au katika maneno ya wimbo wetu, la hasha, upya uwe katika nafasi zetu, roho yetu, akili yetu, utashi wetu. Kristo alituambia divai mpya katika chombo kipya. Sisi leo maisha yetu, maneno na matendo yetu mbele ya Mungu na jirani zetu, aidha katika jumuiya zetu ndo divai, ambayo Yesu Kristo ametujalia kuifanya upya kwa mateso, kifo na ufufuko wake.

Mwimbaji wetu, hana wasiwasi, kwani Mungu ndiye anayeshika usukani wa chombo chetu, na wala si ‘mpigadebe’ katika kituo cha daladala au matatu!. Kutokana na ukweli huu ndio maana anaweza kuuambia ulimwengu uwe na furaha na amani. Kwani haki inatawala kwa wote.

Mzaburi anashadidia umuhimu wa mazingira: miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha, twapaswa kuyapenda na kuyatunza, kwani nayo yana nafasi katika kumsifu Mungu. Kuharibu mazingira ni sawa na kuharibu ala ya muziki wa sifa kwa Mungu, ni ukosefu mkuu. Tunataadharishwa, kwamba twapaswa kumsifu Mungu, kwani tusipomsifu Yeye anayetamalaki nchi, miungu ya uongo itachukua nafasi yake kwa hila, nayo ni ubinafsi, pesa, rushwa, ugomvi, ulevi, uhasherati, umbeya, choyo na ufisadi mwingine mwingi. Kila mmoja wetu katika juma hili kwa maneno na matendo yake, kwa dhati na amhimidi Mungu!


Dominika 3 Mwaka C.
ZABURI 19

Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu,
na anga laitangaza kazi ya mikono yake.
Mchana husemezana na mchana,
usiku hutolea usiku maarifa.

Hakuna lugha wala maneno,
sauti yao haisikilizani.
Sauti yao imeenea duniani mwote,
na maneno yao hata miisho ya ulimwengu.

Katika hizo ameliwekea jua hema,
kama bwana arusi akitoka chumbani mwake,
lafurahi kama mtu aliye hodari
kwenda mbio katika njia yake.
Kutoka kwake lautoka mwisho wa mbingu,
na kuzunguka kwake hata miisho yake,
wala kwa hari yake
hakuna kitu kilichositirika.

Sheria ya Bwana ni kamilifu,
huiburudisha nafsi.
Ushuhuda wa Bwana ni amini,
humtia mjinga hekima.
Maagizo ya Bwana ni ya adili,
Hufurahisha moyo.
Amri ya Bwana ni safi,
huyatia macho nuru.

Kicho cha Bwana ni kitakatifu,
kinadumu milele.
Hukumu za Bwana ni kweli,
zina haki kabisa.
Ni za kutamanika kuliko dhahabu,
kuliko wingi wa dhahabu safi.
Nazo ni tamu kuliko asali,
kuliko sega la asali.

Tena mtumishi wako huonywa kwazo,
katika kuzishika kuna thawabu nyingi.
Ni nani awezaye kuyatambua makosa yake?
Unitakase na mambo ya siri.
Umzuie mtumishi wako asitende mambo ya kiburi,
yasinitawale mimi.
Ndipo nitakapokuwa kamili,
nami nitakuwa safi, sina kosa lililo kubwa.

Maneno ya kinywa changu,
na mawazo ya moyo wangu,
yapate kibali mbele zako, Ee Bwana,
mwamba wangu, na mwokozi wangu.

Zaburi hii inahundwa na zaburi mbili, yaani aya 1-6 na aya 7-14. Sehemu ya kwanza inatukuza utukufu wa Mungu katika mbingu na sehemu ya pili (ambayo ndiyo tunayoiimba katika Dominika hii) inashangazwa na ukuu wa Sheria ya Mungu. Aliyeunganisha sehemu hizi mbili anatuambia kwamba Sheria ya Mungu ni ajabu kuu kama vile utukufu wa upatano tuuonao katika mbingu. Nakumbuka nilipokuwa mdogo, watoto tulipenda kuutazama mwezi usiku, na mara zote tulimwona Mama Bikira Maria katika huo mwezi!

Mzaburi anatupatia visawe sita vinavyoelezea Torati: ni sheria, ni ushuhuda, ni maagizo, ni amri, ni kicho na ni hukumu. Mwamini anapaswa kutii sheria ya Mungu kwani ni kamilifu, huburudisha, uhekimisha, inaudumufu, ni ya haki, kwa yeyote aishikayo ni tamu kama asali. Ama kweli walicholonga wahenga: usigombane na shani ya Mungu! Sheria yake ni ya ajabu, ni ya kushangaza machoni mwetu!

Zaburi hii tunapoipa nafasi ituongoze, inatualika sisi sote kutafakari kwa kina jinsi gani tunavyoiishi sheria ya Mungu. Anga linamvuto kwa watu kutokana na kufuata kwake maongozi ya Muumba. Kila siku asubuhi tunapoamka, tunajua mawio yanatokea upande upi. Mimi na wewe leo, ilikuweza kuwa na upatano na amani katika maisha yetu na katika mahusiano na jirani zetu, twapaswa kufuata amri ya Mungu na hasa kama ilivyohitimishwa na Yesu Kristo (Soma Mt. 22:26 - 40).

Dominika 4 Mwaka C.
ZABURI 71

Nimekukimbilia Wewe, Bwana,
nisiaibike milele.
Kwa haki yako uniponye, uniopoe,
umenitegea sikio lako, uniokoe.
Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu,
nitakakokwenda sikuzote.
Umeamuru niokolewe,
ndiwe genge langu na ngome yangu.

Ee Mungu wangu, uniopoe mkononi mwa mkorofi,
katika mkono wake mwovu, mdhalimu.
Maana ndiwe taraja langu, Ee Bwana Mungu,
tumaini langu tokea ujana wangu.
Nimekutegemea Wewe tangu kuzaliwa,
ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu,
Nitakusifu Wewe daima.

Nimekuwa kitu cha ajabu kwa watu wengi,
na Wewe ndiwe kimbilio langu la nguvu.
Kinywa changu kitajazwa sifa zako,
na heshima yako mchana kutwa.

Usinitupe wakati wa uzee,
nguvu zangu zipungukapo usiniache.
Kwa maana adui zangu wananiamba,
nao wanaoniotea roho yangu hushauriana,
wakisema, “Mungu amemwacha,
mfuatieni, mkamateni, hakuna wa kumponya.”

Ee Mungu, usiwe mbali nami;
Ee Mungu wangu, fanya haraka kunisaidia.
Waaibishwe, watoweshwe, adui za nafsi yangu,
wavikwe laumu na aibu, wanaonitakia mabaya.

Nami nitatumaini daima,
nitazidi kuongeza sifa zako zote.
Kinywa changu kitasimulia haki na wokou wako
Mchana kutwa; maana sijui hesabu yake.

Nitakuja na mambo ya ajabu ya Bwana Mungu,
nitawakumbusha watu haki yako Wewe peke yako.
Ee Mungu, umenifundisha tokea ujana wangu,
Nimekuwa nititangaza miujiza yako hata leo.

Na hata nikiwa ni mzee mwenye mvi,
Ee Mungu, usiniache.
Hata niwaeleze watu wa kizazi hiki nguvu zako,
na haki yako, Ee Mungu, imefika juu sana.
Wewe uliyefanya mambo makuu;
Ee Mungu, ni nani aliye kama Wewe?

Wewe, uliyetuonesha mateso mengi, mabaya,
utatuhuisha tena.
Utatupandisha juu tena
tokea pande za chini ya nchi.
Laiti ungeniongezea ukuu!
Urejee tena na kunifariji moyo.

Nami nitakushukuru kwa kinanda,
na kweli yako, Ee Mungu wangu.
Nitakuimbia Wewe kwa kinubi,
Ee Mtakatifu wa Israeli.
Midomo yangu itafurahi sana nikuimbiapo,
na nafsi yangu uliyoikomboa.
Ulimi wangu utasimulia
haki yako mchana kutwa.
Kwa maana wameaibishwa,
wametahayarika, wanaonitakia mabaya.


Hili ni ombolezo binafsi, kilio cha aliyemzee kwa Mungu. Anaomboleza kwa kuwa amezungukwa na maadui, anakaribia kifo, ni mzee, japo uzee wake haujakausha chemchemi ya matumaini yake, wala kudhoofisha moyo wake wa kidini, kwani akitazama nyuma moyo wake unajaa sifu kwa Mungu ambaye kamwe hajashindwa kumwokoa.

Zaburi hii inaandikwa na mtu ambaye katika maisha yake amekumbana na magonjwa, majaribu makali, maadui na mabalaa kadhaa. Sasa anapokuwa mzee, dhaifu na mpweke maadui zake wanakusanyika kupanga jinsi ya kummaliza kabisa, kwani wanadhani Mungu ameshamtelekeza. Katika wakati huu wa matatizo makubwa, anamwinulia Mungu macho yake, anapaza kwake kilio chake: “genge lake na ngome yake.” Mungu ambaye alikuwa mkunga siku ya kuzaliwa kwake na kuendelea kumwongoza na kumlinda maisha yake yote, kwake ndiye pekee tumaini lake.

Kwa aliye kijana, mzaburi huyu anakuambia jifunze kumsifu Mungu tokea unapokuwa na umri mdogo. Kwa mzee anakuambia kamwe usikate tamaa, Mungu yu pamoja nawe. Kwetu sote, tunaalikwa kutazama jinsi gani tunavyohusiana na wazee, hasa leo tunaposikiwa wastaafu wakinyanyaswa kupata mafao yao, wazee wakikosa matibabu na uwezo wa kujikimu kutokana na uzee wao tu. Wazee wanavyokuwa wapweke kutokana na kuwatenga kwetu. Leo tunaalikwa tuwe kimbilio lao kwa wema wetu kwao!

Papa Yohane Paulo II aliwaandikia wazee barua (1 Oktoba 1999) akionesha mshikamano nao, kwani naye alishakwisha kula chumvi nyingi wakati anaandika barua hii. Papa katika barua hii, anawatia moyo wazee kuishi kikamilifu maisha yao, anatuofundisha thamani ya uzee, lakini hasa anatuasa kuwaheshimu na kuwasaidia katika uzee wao na si kuwanyanyasa na kuwasukuma katika ‘kifo cha huruma’.

Kwa aliye kijana, mzaburi huyu anakuambia jifunze kumsifu Mungu tokea unapokuwa na umri mdogo. Tukumbuke amri ya Mungu: Waheshimu baba na mama, upate miaka mingi na heri duniani! Wazee tulionao katika familia zetu, jumuiya zetu na jamii yetu, ndio wazazi wetu; tunapaswa kuwaheshimu.

Tafakari hii imeandaliwa na Padre Stephano Kaombe.
All the contents on this site are copyrighted ©.