Waamini jengeni utamaduni wa upatanisho ili kukuza na kuimarisha haki na amani!
Askofu mkuu Augustine Kasujja, Balozi wa Vatican nchini Nigeria anawaalika Wakristo
nchini humo kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa kwa njia ya ushuhuda wa
maisha licha ya madhulumu wanayoendelea kukabiliana nayo na kwamba, vitendo hivi visiwakatishe
tamaa, bali waendele kusimama kidete katika imani yao kwa Kristo aliyeteswa, akafa
na kufufuka kutoka katika wafu.
Askofu Kasujja anasema kwamba, katika miezi
ya hivi karibuni, Wakristo nchini Nigeria wamekabiliwa na changamoto kubwa, kiasi
hata cha kutikiswa katika misingi ya imani yao kutokana na madhulumu ya kidini yanayoendelea
kujitokeza sehemu mbali mbali nchini Nigeria.
Wakristo watambue kwamba, ushindi
unapatikana kwa njia ya kukumbatia Msalaba, kama alivyofanya Kristo mwenyewe katika
Fumbo la Pasaka. Kama wafuasi wa Kristo wanatumwa na kuchangamotishwa kuendelea kuwa
ni wajenzi wa misingi ya haki, amani, mshikamano na upatanisho wa kitaifa. Ufalme
wa Kristo uko imara na thabiti, kwani Falme za dunia zitakuja na kutoweka kama ndoto
ya mchana, kama zilivyokuwa tawala mbali mbali za kidunia, jambo la msingi ni Wakristo
kuendelea kutolea ushuhuda imani, matumaini na mapendo.
Askofu mkuu Augustine
Kasujja anasema, Nigeria inahitaji kujenga utamaduni wa haki, amani na upatanisho
wa kitaifa, ili kutoa fursa kwa watu wa dini na madhehebu mbali mbali kuweza kuishi
kwa amani, upendo na mshikamano bila kubaguana kwa misingi ya kidini, kikabila na
mahali anapotoka mtu!