2013-01-19 09:43:42

Udhibiti wa utengenezaji, usambazaji na matumizi ya silaha ujioneshe kwa matendo!


Uamuzi uliochukuliwa hivi karibuni na Serikali ya Marekani kuhusu udhibiti wa usambazaji na matumizi ya silaha ni sahihi kabisa. Takwimu zinaonesha kwamba, wananci wa Marekani wanamiliki kiasi cha silaha millioni 300.

Lakini haitoshi kudhibiti idadi ya silaha zinazomilikiwa na wananchi ili kupunguza mauaji ya kinyama yanayojitokeza mara kwa mara nchini Marekani kama ilivyotokea hivi karibuni huko Newtown na kuwaacha watu wengi wakiwa wameshikwa na bumbuwazi. Mbaya zaidi ingekuwa kwamba, mshangao huu unabaki katika maneno matupu! Matukio haya yametendwa na watu ambao walikuwa na matatizo ya afya ya akili au chuki binafsi, lakini ni matukio yanayotumia silaha za moto!

Viongozi wa kidini 47 wamewaasa Wabunge nchini Marekani kutunga sheria itakayodhibiti matumizi ya silaha za moto yanayofanya watu wasiokuwa na hatia kuendelea kupoteza maisha bila sababu za msingi. Hii ni sehemu ya tahariri ya Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican anayeunga mkono juhudi za Serikali ya Marekani kudhibiti silaha za moto ambazo zimekuwa ni chanzo cha vifo vingi vya watu wasiokuwa na hatia na kwamba, hii ni dhamana ya kiraia na kimaadili.

Wazo la kudhibiti silaha linaweza kupanuliwa na kuwekwa katika medani za kimataifa, hata kama silaha ni kwa ajili ya usalama wa mtu binafsi, lakini bado zimekuwa ni chanzo cha vifo, vurugu na vitisho. Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuweka mikakati ya kudhibiti: uzalishaji, usambazaji na matumizi ya silaha kwani kuna uhusiano mkubwa wa baadhi ya watu kutaka kunufaika na biashara ya silaha au kujitafutia madaraka kwa njia ya biashara ya silaha kimataifa.

Padre Lombardi anasema, mikataba ya kimataifa haina budi kuungwa mkono sanjari na kuendelea kupiga rufuku majaribio na matumizi ya silaha za kinyuklia zinazoendelea kutishia usalama wa maisha ya Jumuiya ya Kimataifa. Jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, wafanyabiashara wataendelea kutengeneza silaha na silaha hizi zitazagaa sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati akiwa safarini kuelekea nchini Lebanon kuzindua matunda ya Sinodi ya Maaskofu Katoliki Mashariki ya Kati, aliungana na wote wanaosikitika kutokana na maafa yanayoendelea nchini Syria, lakini akasema, jambo la kushangaza ni kuona kwamba, hata katika hali tete kama hii, bado watu wanaendelea kupeleka silaha nchini humo.

Padre Federico Lombardi anahitimisha tahariri yake kwa kusema kwamba, amani ya kweli inabubujika kutoka katika undani wa moyo wa mtu! Lakini, amani hii inaweza kufikiwa ikiwa kama kutakuwa na udhibiti mkubwa wa silaha za moto!All the contents on this site are copyrighted ©.