2013-01-19 09:43:20

Mikakati ya kichungaji kutoka Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika ya Kati


Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na mbinu mkakati wa kupata suluhu ya vita nchini DRC ni kati ya mambo yaliyojadiliwa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Kati, lililohitimisha mkutano wake wa Mwaka hivi karibuni, huko Muyinga, nchini Burundi.

Maaskofu wanasema kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa Imani ni kipindi cha neema na baraka na changamoto kwa waamini kuchuchumilia wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha, sanjari na kuhakikisha kwamba, Kanisa linaendelea kuhamasisha ujenzi wa misingi ya haki, amani na utulivu hasa katika nchi zile ambazo bado kuna vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Maaskofu wameibua Mkakati wa pamoja wa shughuli za kichungaji kwa kufanya hija za mshikamano kwa wakimbizi kutoka DRC wanaoishi kwenye Kambi za Wakimbizi nchini Burundi na Tanzania. Maaskofu wanapenda kukuza na kudumisha elimu ya haki na amani katika nchi zao kwa kuendelea kujikita katika dhamana ya upatanisho, changamoto kutoka kwa Mababa wa Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Kati wanataka kuunganisha mikakati yao pamoja na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho.

Maaskofu wanaialika Familia ya Mungu Barani Afrika, kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu; kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu pamoja na kuendelea kuwa ni wajenzi wa amani katika nchi zao, kwa kukataa katu katu sera za chuki, uhasama na ubaguzi, badala yake, kujenga na kuimarisha haki, amani, upendo na mshikamano wa kweli.







All the contents on this site are copyrighted ©.