2013-01-19 11:36:22

Mapadre epukeni kishawishi cha kutafuta mali na uchu wa madaraka!


Askofu mkuu Ignatius Kaigama wa Jimbo kuu la Jos ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria, hivi karibuni alitoa Daraja Takatifu la Upadre kwa Mashemasi sita, na kuwataka Mapadre hao wapya kuchuchumilia kwa namna ya pekee maisha na utume wa Kipadre, unaowapatia fursa ya kuwatakatifuza Watu wa Mungu kwa njia Sakramenti za Kanisa; kuwafundisha Neno la Mungu na kweli za Kiinjili pamoja na kuwaongoza katika hija ya maisha adili, ili siku moja waweze kupata uzima wa milele.

Mapadre wametakiwa kuachana na kishawishi cha kutafuta fedha na uchu wa madaraka; mambo yanayoweza kuwatumbukiza katika malimwengu na hivyo kusahau kutekeleza dhamana na utume wao wa Kipadre, hali itakayowafanya watupu na hatari kwa maisha ya kiroho na utekelezaji wa mikakati ya shughuli za kichungaji ndani ya Kanisa.

Mapadre waridhike na uchaguzi wa wito na maisha yao ya Kipadre, waendelee kuufanyia kazi kwa njia ya Sala, Sakramenti za Kanisa, Tafakari ya kina ya Neno la Mungu pamoja na majiundo endelevu, kamwe waistoe mwanya kwa baadhi ya watu wasiowatakia mema kuvuruga maisha na utume wao wa Kipadre kwa kuwatumbukiza katika malimwengu, huko watakiona cha mtema kuni!

Mapadre wawasaidie waamini kukabiliana na mmong'onyoko wa maadili na utu wema kwa kusimama kidete kupinga udini, utaifa, rushwa, wizi na ubadhirifu wa mali ya umma. Wawe ni kielelezo cha upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa dhidi ya sera na propaganda za kuwagawa watu kwa ukabila, udini na rasilimali za nchi.

Watu washikamane kujiletea maendeleo kiroho na kimwili; wajikite katika ukweli, uwazi na uaminifu; daima wakitafuta mafao ya wengi; tayari kupambana na umaskini, ujinga na maradhi. Kanisa linawahitaji Mapadre watakaojitoa kimasomaso kutangaza Injili ya Kristo, kwa kuwajengea watu Imani, Matumaini na Mapendo.All the contents on this site are copyrighted ©.