2013-01-19 14:22:06

Mali inakabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na vita inayoendelea Kaskazini mwa nchi hiyo!


Askofu mkuu Jean Zerbo, Rais wa Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Mali anaiomba Jumuiya ya Kimataifa kusaidia kutoa msaada wa dharura kwa wananchi wa Mali wanaokabiliwa na vita baada ya Ufaransa na nchi kadhaa za Afrika kutuma vikosi vya ulinzi na usalama nchini humo ili kupambana na vikosi vya kigaidi vinavishikilia eneo la Kaskazini mwa Mali.

Hadi sasa watu zaidi ya watu 400,000 wameyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha na mali zao baada ya mapambano ya silaha kupamba moto Kaskazini mwa Mali. Mwaka 2012 zaidi ya watu millioni 18 walikuwa wanakabiliwa na baa la njaa kutokana na ukame wa muda mrefu. Ongezeko la wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi, linaweza kusababisha tena ukosefu wa chakula, hali inayoweza kuitumbukiza Mali hata katika magonjwa ya mlipuko.

Caritas Mali inahitaji msaada wa dharura kutoka katika Mashirika ya Misaada Kimataifa na Kikanda, ili kuweza kukabiliana na hali ngumu inayowakabili watu wengi nchini humo kwa sasa na kwa siku za usoni. Baadhi ya wananchi wamekimbilia Niger, Burkina Faso na Mauritania.All the contents on this site are copyrighted ©.