2013-01-19 13:31:51

Kanisa litaendelea kumhudumia mwanadamu kiroho na kimwili likiwa aminifu kwa utu na heshima yake!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumamosi, tarehe 19 Januari 2013, amekutana na kuzungumza na Wajumbe wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki Cor Unum, waliohitimisha mkutano wao wa Mwaka hapa mjini Vatican, uliokuwa unaoongozwa na kauli mbiu "Upendo kanuni mpya ya kimaadili na uelewa wa binadamu mintarafu Ukristo".

Anasema, ushuhuda wa huduma ya upendo inayotekelezwa na waamini unaweza kuwa ni mlango wa imani kwa wale ambao wanamtafuta Yesu katika maisha. Maadili mintarafu Ukristo yanapata maana yake kwa mwamini kuonja upendo wa Yesu Kristo, unaomwezesha mwamini huyo kuwa na mwelekeo mpya unaompatia dira na mwongozo wa maisha. Upendo wa Kikristo unabubujika kutoka katika imani inayowabidisha Wakristo kujitoa kimasomaso kwa ajili ya wengine.

Baba Mtakatifu anasema, imani inayojionesha katika upendo ni kati ya mambo msingi yanayompatia mwamini mang'amuzi na utekelezaji wa utume wake katika Mashirika na vyama vya misaada inayotolewa na Kanisa, kama njia ya kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Mwamini mwenye imani thabiti anakuwa pia na vigezo makini vya kupima mchakato wa umwilishaji wa upendo katika hali halisi inayomzunguka.

Mwanadamu kwa bahati mbaya katika karne iliyopita amejikuta akitumbukia kwenye utumwa wa mawazo kutokana na sera na siasa ambazo zilijikuta zikikumbatia utaifa, mbari, tabaka la kijamii na hivyo kupewa kipaumbele cha kwanza. Ubepari unaotafuta faida kubwa umesababisha athari kubwa za myumbo wa uchumi kimataifa, matabaka na umaskini mkubwa. Kuna haja ya kusimama kidete kutetea na kulinda utu na heshima ya binadamu ambao una mafao makubwa kwa utamaduni na katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa upendo.

Baba Mtakatifu anasema, kwa bahati mbaya, watu wengi wameshindwa kutambua mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu na badala yake wamemezwa na malimwengu na kile kinachodaiwa kuwa ni maendeleo ya sayansi na teknolojia, matokeo yake ni ukanimungu, kwa kudhani kwamba, mwanadamu anaweza kujitegemea mwenyewe bila ya uwepo wa Mungu.

Mawazo kama haya yanaendelea kuibua sera tenge za udhibiti wa idadi ya watu na kumkuza mwanadamu kuliko hata ile nafasi yake ya kawaida, kwa kudhani kwamba, kwa njia hii ataweza kujipatia furaha ya kweli, lakini, ukweli wa mambo ni kwamba, anapinga asili yake kama kiumbe aliyeumbwa na Mwenyezi Mungu, matokeo yake ni mwanadamu kuzungukwa na upweke wa kutisha na kukatisha tamaa.

Baba Mtakatifu anasema, imani inamwezesha mwamini kuwa na mwono wa kinabii, ili kukabiliana na mmong'onyoko wa kimaadili na mawazo yanayozunguka katika mwelekeo kama huu. Kanisa halina budi kuendelea kuwa ni mhimiri wa ukweli hata pale linaposhirikiana na Mashirika ya Kimataifa katika utoaji wa huduma, dhidi ya sera na siasa zinazohatarisha utu na heshima ya binadamu.

Hii ni changamoto pia kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa na mwono makini kuhusu binadamu na haki zake msingi. Kanisa litaendelea kumhudumia mwanadamu mzima: kiroho na kimwili, kadiri ya Mpango wa Mungu. Huu ndio mwelekeo sahihi pia kwa Taasisi na Mashirika ya huduma ya Kanisa: utu na heshima ya binadamu mwenye muungano wa dhati na Mwenyezi Mungu, anaonesha: unyenyekevu na imani na kwamba, mwanadamu si kisiwa bali utimilifu wake unaojionesha katika uhusiano wake na Jamii.

Mama Kanisa ataendelea kuunga mkono utu na heshima ya ndoa kati ya Bwana na Bibi kama kielelezo cha hali ya juu cha uaminifu kati ya mwanaume na mwanamke. Anapinga falsafa tenge zinazotetea usawa wa kijinsia kwani utofauti wa kijinsia ni kielelezo asili cha kukamilishana kadiri ya mpango wa Mungu.

Baba Mtakatifu anawapongeza na kuwashukuru wajumbe wote wa Cor Unum kwa kujitoa kimaso maso kwa ajili ya kumhudumia mwanadamu, daima wakiwa waaminifu kwa utu na heshima yake. Changamoto zinazoendelea kutolewa katika ulimwengu mamboleo zinaweza kupata jibu lake kwa kukutana na Kristo anayempatia mwanadamu utimilifu wa maisha yake; daima akiwa mstari wa mbele kutafuta mafao yake binafsi na yale ya wengi. Hii ndiyo njia sahihi inayopaswa kufuatwa katika utoaji wa huduma.All the contents on this site are copyrighted ©.