Umoja wa Wakristo ujikite katika tafakari ya kina kuhusu Mafundisho Tanzu ya Kanisa
na ushuhuda katika huduma
Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Umoja wa Wakristo
katika maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican sanjari
na Mwaka wa Imani anabainisha kwamba, tafsiri sahihi na makini ya Mtaguso Mkuu wa
Pili wa Vatican ni tukio rejea kwa Kanisa Katoliki katika mageuzi yanayoendelea kutekelezwa
na Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Kiini cha mabadiliko
haya yanajionesha kwa namna ya pekee, katika Maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa. Hapa
unaweza kubainisha mageuzi ndani ya mageuzi. Tafsiri na ufahamu mpana zaidi wa Nyaraka
za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ni muhimu sana katika kugundua na kuenzi utajiri
uliomo kwenye Nyaraka kumi na sita za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ili uweze kutumika
katika kuendeleza maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Mageuzi
ya Kiliturujia hayana budi kutazamwa katika Maadhimisho yote ya Mtaguso Mkuu wa Pili
wa Vatican na tasiri yake makini, vinginevyo, watu wanaweza kujikuta kwamba, wanapoteza
dira na lengo la Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kwa maisha na utume wa Kanisa. Mwaka
wa Imani uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita unalandana
sana na Mwaka wa Imani uliotangazwa na Papa Paulo wa sita; kwani viongozi hawa wa
Kanisa wanatumia Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kama rejea ya maadhimisho ya Mwaka
wa Imani. Kwa Papa Paulo wa sita, Mwaka wa Imani yalikuwa ni matokeo ya maadhimisho
ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita,
ameutangaza Mwaka wa Imani, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso
mkuu wa Pili wa Vatican. Ni mwaliko na changamoto ya kutangaza na kutolea ushuhuda
Imani kwa Kristo na Kanisa lake, kama njia ya kukabiliana na changamoto, vikwazo na
fursa zinazoendelea kujitokeza katika Ulimwengu mamboleo. Waamini wanachangamotishwa
kwa njia ya ushuhuda wa imani katika matendo, kuyatakatifuza malimwengu: kwa mwanadamu
kuheshimiwa na Mungu kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha. Maadhimisho ya
Mwaka wa Imani anasema Kardinali Kurt Koch yana umuhimu wa pekee katika majadiliano
ya Kiekumene na Waamini wa dini ya Kikristo. Umoja wa Wakristo unaweza kupatikana,
ikiwa kama Wakristo kwa pamoja wataweza kufanya tafakari ya kina kuhusu Mafundisho
Tanzu ya Kanisa na Misingi ya Imani ya Kanisa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, katika
ukame na jangwa la maisha ya watu: kimaadili na kiutu, kuna haja ya kuwa na ushuhuda
wa pamoja unaotolewa na Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Mageuzi ya Kiliturujia
yaliyofanywa na Kanisa Katoliki ni mada inayofuatiliwa na Makanisa na Madhehebu mengine
ya Kikristo, kwani wanataka kufahamu maana na umuhimu wake katika maisha na utume
wa Kanisa. Mageuzi ya Kiliturujia yanayofanywa na Kanisa Katoliki yanajikita katika
Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Mageuzi haya yanafumbata
kwa namna ya pekee Mapokeo ya Kanisa. Kardinali Kurt Koch anafafanua zaidi kwa
kusema kwamba, ifahamike kuwa mabadiliko ya Kiliturujia yaliyoletwa na Mtaguso Mkuu
wa Pili wa Vatican, hayamaanishi kujitenga na Historia, Mapokeo na Urithi wa utajiri
wa Kanisa kwa miaka iliyopita. Bali haya ni maboresho ya maisha na utume wa Kanisa,
katika kusoma alama za nyakati, maneno yaliyopewa msukumo wa pekee na Mababa wa Mtaguso
Mkuu wa Pili wa Vatican, kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu; kulinda
na kutetea ut una heshima ya mwanadamu; kutafuta mafao ya wengi; haki, amani na mshikamano;
Mwenyezi Mungu akipewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na mikakati ya binadamu
katika ulimwengu mamboleo.