2013-01-18 08:11:04

Tafakari ya Neno la Mungu: Siku ya kwanza ya kuombea Umoja wa Wakristo


Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo kwa Mwaka 2013 linaoongozwa na kauli mbiu ”Kile ambacho Bwana anataka kutoka kwetu” sehemu ya ujumbe wa Nabii Mika 6:6-8. Kwa hakika Bwana anawaalika waja wake kutenda hakli, kupenda rehema na kutembea katika fadhila ya unyenyekevu.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anawaalika Wakristo wote kuwa wadumifu katika kuombea umoja wa Wakristo, wakiongozwa na Roho Mtakatifu, ili kwa pamoja waweze kuungama kwamba Yesu Kristo ni Mkombozi wa ulimwengu, wakishikamana ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuibuka katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Tunalianza wiki la sala kuombea umoja wa Wakristo Mada inayotuongoza wiki nzima ni kutembea na Mungu katika mazingira yote. Katika siku hii ya kwanza wazo letu kuu ni kuongea na Mungu tukitembea katika njia ya imani

Kuwa wanyenyekevu kwa Mungu maana yake kutembea kama mtu anayeongea na mtu mwingine au na Mungu mwenyewe, daima makini kwa kile tunachokisikia. Tunaanza wiki la sala kwa ajili ya kuombea umoja wa kanisa tukiwa na mantiki ya kushirikishana Neno la Mungu,kusoma Biblia ambayo ni mhimili na kifungamanisho cha mazungumzo na umoja wa kiekumene.
Wakati huu tunapata fursa ya kufungua nafsi zetu kwa ajili ya kujifunza kutoka kwa wengine, kushirikiana katika kile tulicho nacho kwa pamoja bila kuacha kusikiliza kile ambacho tunatofautiana. Kwa njia hii tunapata kuelewana na kuendelea mbele katika kile ambacho Mungu anatutaka tufanye. Tunatenda haki na ukarimu kwa kukaa pamoja kuongea na kusali. Umaskini wa kutengwa unaondolewa kwa namna hii.
Neno la Mungu siku ya leo linatuonyesha kuwa Mungu hana kiburi au ubinafsi katika kutenda kwake yaani hajijengea jina mwenyewe kama watu wa mnara wa Babeli. Roho mtakatifu wa Mungu ni utajiri unatuunganisha wanadamu wote tusiwe pweke. Roho huyu anatufundisha sanaa ya kuwasikiliza wengine, kuwajengea jina wengine.
Simulizi tulilolisikia linaeleza ni kwa jinsi gani tunaweza kushikamana kama msingi wa kujitangaza mwenyewe. Kwa njia ya pentekoste, yaani kumiminiwa Roho Mtakatifu na kupitia nguvu ya ufufuo wa Yesu maelewano yanawezekana licha ya tofauti zetu. Sisi tumealikwa kushiriki kusikiliza zawadi ya hotuba inayotuelekeza kwa Bwana, na kuelekea uhuru. Tumeitwa kutembea katika Roho.
Tunasali pamoja kwa sababu tunahitaji kwenda pamoja katika hali inayojitokeza ya kupoteza matumaini na kukata tamaa. Ni mawasiliano ambayo yanajikita katika mantiki ya kwenda kwa pamoja lakini pia katika muktadha wa kupoteza matumaini na kukata tamaa. Kama makanisa yanayoishi katika hali ya utengano na jamii iliyomegwa kwa chuki na hofu ya mtu mwingine.
Tunaweza kujitambua katika hali hii. Ni hapa hasa ambapo Yesu anachagua kuungana nasi katika mazungumzo yetu kama alivyofanya kwa wafuasi wa Emmaus. Yeye hatwai hali ya anayeamuru au kufundisha bali kutembea kandokando ya mfuasi. Ni hamu yake kuwa sehemu ya mazungumzo yetu na jibu letu la kumtaka akae nasi na kuongea zaidi nasi ili atuwezeshe kumuona yeye aliye Bwana wa ufufuko.
Wakristo wote wanajua kitu fulani juu ya kukutana na Yesu na nguvu ya neno lake linalowaka ndani yetu. Neno hili ambalo ni matunda ya maisha ya ufufuko linatuita kuungana na Kristo kwa ndani zaidi. Mazungumzo ya daima kati yetu na Yesu - hata wakati tunapoteza njia yanatusaidia sana kutuunganisha na kutuweka pamoja.

SALA

Ee Bwana Yesu Kristo tunakiri kabisa kwamba sisi ni watu wako tunakushukuru kwa kutualika kuongea nawe kwa upendo. Ifungue mioyo yetu iweze kushiriki kikamilifu katika sala yako kwa Baba yako ili tuwe kitu kimoja katika safari yetu kuja kwako. Tuwezeshe kukaa karibu daima. Tupe ujasiri wa kushuhudia ukweli pamoja. Tunaomba sala zetu ziwakumbatie wale wanaoomba na kuudumisha umoja. Mtume Roho wako mtakatifu atutie nguvu ya kupambana na hali ambayo inadharau heshima na huruma ndani ya jamii, mataifa na ulimwengu. Wewe uliye wa haki tuongoze katika njia ya haki na amani. Amina.


MASWALI:

1. Ni wapi tunaongea kikweli katikati ya tofauti zinazotutenganisha?
2. Je, mazungumzo yetu yanalenga mipango yetu binafsi au maisha yanayoleta matumaini?
3. Ni watu gani tunaongea nao na tunawataka tuongee nao? Kwanini? Tukiwa na wazo hili tunasherehekea fumbo la kujikomboa kiuhuru, yaani kutafuta uhuru, ambalo linatukia hata katika sehemu ambamo nyanyaso, chuki na umaskini uliotopea vinaonekana kuwa ni mzigo mkubwa?
Imeandaliwa na Padre Emmanuel Nyaumba.

All the contents on this site are copyrighted ©.