2013-01-18 07:19:55

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa: Mkaribisheni Yesu katika Familia zenu kwani ni chemchemi ya furaha ya kweli!


Mpendwa mwana wa Mungu, Dominika iliyopita tulisherehekea Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, sikukuu ambayo ilihitimisha kipindi cha Noel na shamrashamra za Mwaka Mpya. Ni sikukuu ambayo pia huchukua nafasi ya Dominika ya kwanza ya kipindi cha kawaida cha Mwaka wa Kanisa, kumbe leo tunatafakari masomo ya Dominika ya II ya kipindi cha mwaka Che wa Kanisa. ambayo yatuongoza kutambua kuwa Bwana yu katikati yetu na ndiyo furaha yetu. RealAudioMP3

Nabii Isaya katika somo la kwanza anatangaza upendo wa Mungu kwa taifa la Israel. Kama tunavyofahamu, Mungu alimwahidi mfalme Daudi kuwa katika ukoo wake utatokea mwangaza utakaokuwa kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu. Kwa zawadi hii kwa mfalme Daudi watu wote watauona utukufu wa Mungu. Nabii Isaya anatoa mfano wa Bwana na Bibi arusi wanavyopendana ndivyo ambavyo Mungu analipenda taifa la Israeli na watu wake wote. Kwa zawadi hii, mzaburi wa Zaburi ya 95 anatualika kumwimbia Bwana wimbo mpya na kuhubiri habari za utukufu wa Mungu kwa mataifa yote

Mtume Paulo anapowaandikia Wakorinto katika somo la pili anataka kusisitiza nguvu ya Mungu Roho Mtakatifu anayegawa vipaji vyake kadiri apendavyo kwa kila mmoja wetu. Kwa kugawa vipaji kwa kila mmoja anataka kutuonjesha uzuri wa maisha ya jumuiya, maisha ya kusaidiana. Ndiyo kusema vipaji si zawadi binafsi bali ni kwa ajili ya kuwafaidia wengine. Mtume Paulo anasema, pana tofauti ya karama lakini mgawaji wa mapaji hayo ni mmoja yaani Roho Mtakatifu.

Mama Kanisa katika hili daima yuko makini kuongoza taifa la Mungu ili lisije likaanguka katika kiburi cha majivuno! Katika historia na hata zama zetu wapo baadhi yetu ambao hujisikia kama vile wao ndio Roho Mtakatifu! Kwa kutafakari somo hili tunaalikwa kuwa makini katika kutumia zawadi tulizopewa na hasa kwa ajili ya kufaidia taifa la Mungu na si kwa faida binafsi.

Mpendwa mwana wa Mungu sehemu ya Injili tunayoitafakari leo yaani Injili ya Yohane 2:1-12 tunasikia habari ya arusi ya Kana ya Galilaya. Kristo aliyejitangaza waziwazi katika sherehe ya Tokeo la Bwana anazidi kujionesha wazi katika umungu wake na unyenyekevu wake, na zaidi katika uchungaji wa taifa lake.

Mpendwa mwanatafakari, hebu tujiulize, kama ingetokea mtu mmoja akamwuliza Myahudi, wapi Mungu anaishi au wapi tunaweza kukutana na Mungu, unatarajia Myahudi huyu angejibu nini? Kwa vyovyote vile Myahudi angesema Mungu anakaa katika Hekalu la Yerusalemu au anakaa mlimani! Leo baada ya kusikia sehemu ya Injili ya Yohane juu ya arusi ya Kana ukiulizwa utatoa jibu lilelile la Myahudi?

Natumaini jibu letu linapaswa kuwa kama inavyojionesha katika Injili, yaani Mungu tunaweza kumpata mezani petu tunapokula chakula, katika sherehe yetu ya ndoa na katika Misa Takatifu. Kumbe, tunaweza kusema kuwa arusi ya Kana ni kielelezo cha uwepo wa Bwana katikati ya maisha yetu, ambaye ndiye yule Emanueli, yaani Mungu pamoja nasi. Bwana yu katikati ya watu wanaofurahi na kuchangamka katika maisha yao.

Katika arusi ya Kana Bwana anafungua namna mpya ya kuwa katikati ya waamini, anafurahi na waamini na si tu katika furaha ya kiroho bali pia katika furaha inayogusa maisha ya kawaida. Jambo la namna hii latukumbusha fikira za Mtakatifu Katarina wa Siena aliyekuwa akimwomba Mungu atuondolee maisha yanayojionesha katika sura zilizojaa huzuni! Kwa tendo la Bwana pale Kana hali ya maisha ya watu imeinuliwa juu ili yawe kweli maisha ya furaha.

Katika arusi ya Kana tunaona jambo jingine la kutufanya tufikiri na kutafakari juu ya maisha yetu na uwezo wa Mungu kati yetu. Jambo lenyewe ni kuishiwa Divai. Wote twafahamu kuwa Divai ni alama ya furaha na shamrashamra katika maisha ya Kiyahudi. Kwisha kwa Divai maana yake kwisha kwa furaha! Bwana yupo pale pamoja na wanaarusi, anaona Divai imeisha!

Hapa twajifunza kuwa Yesu hayuko pale kushiriki furaha tu bali hata kupokea na kushiriki machungu ya maisha ya watu. Hata hivyo atabadirisha machungu haya na kuyafanya yawe furaha! Anageuza maji na kuwa divai. Mpendwa mwujiza wa kwanza! Divai ni nzuri kupindukia na furaha inatokea si kinyume cha furaha ya mwanzo bali anakamilisha furaha hiyo. Mpendwa Bwana aweza kubadili maisha yako ya uchungu kuwa furaha, cha msingi mwambie Maria, sina divai!

Mama Maria anawaambia watumishi fanyeni yale atakayosema na wanafanya hivyo! Sisi leo tunaalikwa kufanya anayosema Bwana katika Neno lake na hapo ndipo kuna furaha sasa na hata milele. Katika kupata furaha hii tunahitaji kushiriki kikamilifu kazi nzima hata kama ni ngumu! Divai ya furaha ni tunda la kushirikishana pamoja vipaji kati ya watu mbalimbali.

Tunamwona Mama wa Mungu, watumishi wa sherehe, mwenye kuongoza arusi kila mmoja anafanya sehemu yake kadiri ya kipaji alichopewa na Mungu kadiri tulivyosikia katika somo la II, Mtume Paulo akifundisha juu ya karama zitokazo kwa Roho Mtakatifu kwa ajili ya kufaidiana. Mpendwa yafaa tukumbuke kwamba kitovu cha furaha yote baada ya kushirikishana yote ni Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye kadiri ya Nabii Isaya ndiye ambaye hawezi kumwacha awaye yote katika taabu bali atamfanya angae mbele ya mataifa.

Ninakutakieni furaha tele katika maisha yako ukikumbuka kuwa Bwana ndiye mchungaji mwema, ndiye chanzo na mwisho wa furaha na amani ktk maisha yetu na daima ukimwalika pamoja na Mama Maria atakuwa nawe kukuinua na kukusaidia ukakue katika furaha na kisha uzima wa milele. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya, C.PP.S.

All the contents on this site are copyrighted ©.