2013-01-18 09:00:21

Msifanye utume wenu kwa mazoea, wala kutopea katika maraha ya dunia; bali muwe ni watu wenye imani thabiti kwa kujitoa kwa Mungu na jirani!


Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican, katika maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Anthony Abate, hapo tarehe 17 Januari 2013 ameshiriki katika masifu ya jioni pamoja na Jumuiya ya Taasisi ya Diplomasia ya Kanisa, kwa kuwakumbuka Mabalozi na wasaidizi wao wanaotekeleza wajibu wao sehemu mbali mbali za dunia, bila kuwasahau wale ambao wametangulia mbele ya haki wakiwa na tumaini la ufufuko na kwa namna ya pekee, Askofu mkuu Ambrose Madtha, aliyefariki kwa ajali ya gari wakati akitekeleza utume wake kama Balozi wa Vatican nchini Pwani ya Pembe, hivi karibuni.

Katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Kardinali Bertone anasema, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anawaalika waamini wote kufanya hija ya imani kwa kutafuta yale mambo msingi katika maisha yao ya Kikristo, kwa kuwaonjesha wote wanaokutana nao ile furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Ni changamoto ya kutubu na kumwongokea Kristo Mkombozi wa Ulimwengu.

Uwe ni mwaka wa neema hata kwa wale wanaotekeleza wajibu wao kama wawakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro sehemu mbali mbali za dunia, kwa kujitoa kimasomaso kumfuasa Kristo kwa njia ya huduma yao makini; wakitambua changamoto, vikwazo na fursa ambazo ziko mbele yao. Kamwe wasifanye kazi kwa mazoea wala kutopea katika maraha ya duniani, bali wawe ni watu wenye imani inayosimikwa katika misingi mikuu miwili: yaani Mwenyezi Mungu na Mafundisho Tanzu ya Imani.

Maisha yao kama Wahudumu wa Injili ya Kristo yaboreshwe kwa njia ya: Sala, tafakari ya Kina ya Neno la Mungu; Majiundo endelevu kuhusu kweli za Imani, ili kweli Maadhimisho ya Mwaka wa Imani yaweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, yaani wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.

Watambue kwamba, pale ambapo Mwenyezi Mungu anapewa utukufu, mwanadamu pia anaheshimiwa na kuthaminiwa. Wao pia wajitahidi kuwa ni wajenzi wa amani, upendo na mshikamano wakianzia katika maisha yao binafsi, Jumuiya wanamoishi na katika medani mbali mbali za utume wao ndani na nje ya Kanisa. Wao kama viongozi wa Kanisa wanahifadhi Urithi wa Imani, changamoto ya kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani; daima wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa mtu na mahitaji yake msingi.

Wanafunzi katika taasisi hii anasema Kardinali Bertone, watambue kwamba, wanaundwa kwa ajili ya Kanisa zima na kwa namna ya pekee, kuwa ni wawakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika utekelezaji wa dhamana na utume wake. Ni mwaliko wa kujenga na kuimarisha imani, umoja na matumaini katika wito na maisha yao kama Mapadre.

Wajitambulishe na Kristo pamoja na Kanisa lake; wakijitahidi kujenga na kuimarisha mshikamano wa umoja, upendo na mshikamano kati yao. Kama binadamu wafahamu karama na mapungufu yao ya kibinadamu, daima wakiwa na ujasiri wa kukabiliana vikwazo na changamoto mbali mbali za maisha. Wajitahidi kuwa waaminifu kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, wakitolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.All the contents on this site are copyrighted ©.