2013-01-18 07:41:07

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, yaamshe imani kwa Kristo na Kanisa lake!


Patriaki Nerses Bedros XIX wa Warmeni Wakatoliki, hivi karibuni ameungana na Familia ya Mungu, Jimbo la Beirut, Lebanon kwa ajili ya kuadhimisha Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita. Katika mahubiri yake, Patriaki Nerses Bedros XIX amesisitiza kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa Imani yanapania kwa namna ya pekee kuamsha imani kwa Kristo na Kanisa lake. RealAudioMP3

Kunako Karne ya IV, Mtakatifu Gregori alijibidisha kutangaza Injili ya Kristo na watu wengi kutoka Armenia wakatubu, wakaongoka na kubatizwa na hivyo kuuona ule mlango wa imani unaowafungulia uzima wa milele kwa njia ya Maji na Roho Mtakatifu. Warmeni Wakatoliki tangu wakati huo wamekuwa mstari wa mbele kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kiasi hata cha kutolea maisha yao, ili yaweze kuwa ni sadaka na mbegu ya kueneza Ukristo, kama ilivyotokea kunako mwaka 1915 wakati wa mauaji ya kimbari.

Katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, waamini wanapaswa kujiuliza ni kwa jinsi gani wameendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake na jinsi ambavyo wanaendelea kujibidisha ili kurithisha Imani hii kwa vijana wa kizazi kipya, wanaokabiliwa na changamoto mbali mbali za kiimani, kimaadili na kiutu.

Patriaki Nerses Bedros XIX anasema, Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, yapanie kuwashirikisha na kuwaonjesha wengine ile furaha ya kumwamini Kristo Mkombozi wa dunia, aliyezaliwa, akateswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hivyo kumwonjesha huruma na upendo wa Mungu, ili hatimaye, kumshirikisha maisha ya uzima wa milele. Yesu Kristo aliyemwaga Damu yake azizi pale Msalabani, anapenda kuwashirikisha watu wote zawadi ya ukombozi.

Kumbe, ni dhamana na jukumu la kila mwamini kuendelea kujibidisha kutangaza Injili ya Kristo hadi miisho ya dunia, kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao katika medani mbali mbali za maisha. Lakini, familia inapaswa kuwa ni shule ya kwanza ya Uinjilishaji Mpya, mahali pa kurithisha imani, matumaini na mapendo; ili kwamba, moto huu uweze kuenea na kusambaa kwa wale ambao bado hawajabahatika kusikia Injili ya Kristo ikitangazwa katika viunga vyao. Vijana wahusishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, ili hapo baadaye, waweze kuendeleza dhamana ya kutangaza Injili ya Kristo.

Waamini watambue kwamba, kabla ya Kuinjilisha wengine, wao wenyewe wanapaswa kujiinjilisha na kukoleza maisha yao kwa njia ya Imani ya Kikristo kama inavyopembuliwa vizuri katika Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki. Maisha yao yakolezwe na utakatifu wa maisha kwa njia ya neema na baraka zinazobubujika kutoka katika Sakramenti za Kanisa. Kwa njia hii, waamini wataweza kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya maisha yao adili, yanaoongozwa na Amri kumi za Mungu. Yote haya yanafumbatwa pia katika Sala na kumwilishwa katika matendo ya huruma na mapendo kwa jirani na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Waamini watumie fursa mbali mbali zinazotolewa na Mama Kanisa katika kujisomea, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha. Katika hija ya imani na maisha ya Kikristo, Kanisa katika nyakati mbali mbali, limebahatika kupata watakatifu na mashahidi walioungama imani yao kwa njia ya sadaka kubwa. Ni jukumu la waamini kuiga mifano ya watakatifu hawa, kama njia ya kukoleza Imani katika mazingira ya watu wa nyakati hizi.

Patriaki Nerses Bedros XIX anahitimisha mahubiri yake katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa kuwakumbusha waamini kuwa, daima wanapotangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, watambue kwamba, wanajenga na kuimarisha moyo wa upendo na mshikamano; haki na amani na kwamba, imani ina thamani kubwa zaidi kuliko hata fedha ambayo kwa sasa inaonekana kutawala maisha ya watu.

Imani ina umuhimu wa pekee kuliko hata uchu wa madaraka unaoyatumbukiza mataifa mengi katika migogoro, kinzani na vita; imani ina nafasi ya pekee kuliko hata sayansi, kwani kwa njia ya Imani, mwamini anaweza kuhamisha milima. Waamini wawe na unyenyekevu katika hija ya maisha yao, kwa kumwomba Yesu Kristo ili aweze kuwaongezea imani, kama walivyofanya Mitume, pale walipoonesha wasi wasi na mashaka.
All the contents on this site are copyrighted ©.