Baraza la Maaskofu Katoliki Italia limeanza hija ya kitume mjini Vatican, inayofanyika
walau kila baada ya miaka mitano, ili kutoa taarifa ya maisha, utume na mikakati ya
majimbo kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na Mabaraza ya Kipapa.
Maaskofu
wa Italia wanafanya hija hii wakati ambapo Italia inakabiliwa na changamoto za kiuchumi,
kisiasa, kijamii, kimaadili na kiutu. Takwimu zinaonesha kwamba, Italia imeendelea
kukabiliwa na hali ngumu ya uchumi kuanzia mwaka 2009 hadi wakati huu.
Hii
ni kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, zilizopelekea ukuaji wa uchumi
wa Italia kudorora kwa kiasi kikubwa na hivyo deni la taifa kuongezeka kwa asilimia
120%. Tatizo la ajira nchini Italia, kwa sasa ni asilimia 11%, lakini waathirika wakubwa
ni vijana. Kutokana na kushuka kwa soko la ndani na nje, makampuni na viwanda vingi
vimejikuta vikilazimika kufunga shughuli zake za uzalishaji au kuhamia katika nchi
nyingine, wakiwa na tumaini la kupata walau faidia kidogo kutokana na kupanda mno
kwa gharama za uzalishaji nchini Italia na Jumuiya ya Ulaya katika ujumla wake.
Waziri
mkuu Mario Monti na Serikali yake ya kipindi cha mpito, katika kipindi cha mwaka mmoja
uliopita, ililazimika kubuni mbinu mkakati wa kupunguza matumizi, kuongeza pato, kudhibiti
ukwepaji kodi pamoja na kurudisha imani kwa wawekezaji kutoka ndani na nje ya Italia.
Huu ni mkakati ambao umewalazimisha wananchi wengi wa Italia kujifunga kibwebwe ili
kukabiliana na hali ngumu ya maisha, kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha wakati
huo hali ya maisha ikishuka kwa kasi kubwa, kutokana na watu wengi kukabiliwa na hali
ya umaskini wa kipato kutokana na ukosefu wa fursa za ajira. Hali ya umaskini ni mbaya
zaidi kwa familia zenye watoto zaidi ya mmoja.
Itakumbukwa kwamba, tarehe 11
Februari 1929, Serikali ya Italia, chini ya uongozi wa Benito Mussolini na Kardinali
Pietro Gasparri, Katibu mkuu wa Vatican, pande hizi mbili ziliwekeana Mkataba unaojulikana
kuwa ni Mkataba wa Laterano, ambao ulitoa uhuru kamili wa Vatican kuwa ni nchi inayojitegemea
katika mambo yake. Serikali ya Italia, ikakubaliana na kushirikiana na Kanisa katika
masuala ya kidini, sheria za ndoa pamoja na sekta ya elimu.
Kunako tarehe 18
Februari 1984, Waziri mkuu wa wakati huo, Bertino Craxi kwa niaba ya Serikali ya Italia
na Kardinali Agostino Casaroli kwa niaba ya Vatican walifanya marekebisho makubwa
katika Mkataba wa Laterano. Dini ya Kikatoliki iliyokuwa inatambuliwa kuwa ni dini
ya Serikali na Nchi ya Italia kwa ujumla, ikaondolewa katika Katiba ya Nchi, ili kutoa
uhuru wa kidini kwa waamini wa dini na madhehebu mbali mbali nchini Italia.
Uteuzi
wa Maaskofu wa Italia, ukawa unafanywa moja kwa moja na Khalifa wa Mtakatifu Petro,
bila kuhitaji kwanza kibali kutoka Serikali ya Italia. Kuhusiana na masuala ya fedha
na uchumi, waamini na wananchi wenye mapenzi mema, wakapewa uhuru wa kuchangia katika
utume wa Kanisa kadiri ya sheria za nchi. Utekelezaji wa mpango mkakati huu ukaanza
kunako mwaka 1987. Na fedha inayotolewa na waamini pamoja na wananchi wenye mapenzi
mema kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa inadhibitiwa kikamilifu na Kanisa
pamoja na Sheria za Nchi.
Hii ndiyo fedha ambayo Baraza la Maaskofu Katoliki
Italia, limekuwa likitumia kwa ajili ya kusaidia kugharimia miradi mbali mbali ya
maendeleo katika Makanisa ya Kimissionari sehemu mbali mbali za dunia na msaada wa
dharura kwa watu wanaokumbwa na majanga asilia. Baraza la Maaskofu Katoliki linawajibika
kutoa taarifa ya fedha zilizokusanywa na matumizi yake. Sheria hii pia inayahusu Madhehebu
mengine ya Kikristo yanayotekeleza utume wake nchini Italia.
Utafiti na upembuzi
wa kina uliofanywa kuhusiana na tunu msingi hususan: maisha, familia, kazi, dini,
siasa na jamii zinabainisha kwamba, wananchi wengi wa Italia bado wana mwamko wa imani
kwa Kanisa Katoliki, ikilinganishwa na nchi nyingine 48 kutoka Ulaya.
Bado
kuna waamini wanaoshiriki kikamilifu katika Ibada zinazofanyika kila juma, ingawa
pia kuna asilimia ishirini ya watu ambao kwa sasa wameshindwa kuona tena mlango wa
Kanisa. Tatizo kubwa linalojitokeza kwa sasa ni kuhusiana na kweli za Kiimani, uhusiano
na taasisi za kidini na kile mwamini anacho amini kutoka katika undani wa maisha yake.
Kwa
ufupi, hii ndiyo hali halisi ya maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini Italia,
wakati huu Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, linapoendelea na hija yake ya kitume
mjini Vatican.