2013-01-17 11:00:31

Mwanadamu ana kiu kubwa ya uwepo wa Mungu katika maisha yake; kinyume chake ni mateso, taabu na mahangaiko na kilio!


Kardinali Robert Sarah, Rais wa Baraza la Kipapa linaloratibu Misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum anabainisha kwamba, mwanadamu ana kiu ya uwepo wa Mungu katika maisha yake, kukosekana kwa Mungu kumepelekea taabu na mateso makubwa miongoni mwa watu sehemu mbali mbali za dunia.

Mkutano wa Cor Unum unaonza tarehe 17 hadi 19 Januari 2013 hapa mjini Roma, ni fursa ya kuwashukuru wadau mbali mbali wanaojitoa kimaso maso kwa ajili ya huduma ya upendo kwa jirani na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Misaada inayotolewa na wadau mbali mbali ilenge kuleta mabadiliko katika maisha ya watu na kamwe isiwe ni kikwazo katika kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu, kwani mara nyingi Mashirika ya Misaada Kimataifa yamekuwa yakitoa misaada yenye masharti magumu kama njia ya kudhibiti idadi ya watu pamoja na kutaka kuhalalisha kile kinachodaiwa kuwa ni haki msingi za kibinadamu, hata kama zinakwenda kinyume cha utu na maadili mema.

Bara la Afrika linapaswa kuwa makini zaidi na sera zinazopigia debe kuhusu "uwezeshaji wa wanawake na usawa wa kijinsia mambo ambayo yanataka kumpatia mwanadamu uhuru usiokuwa na mipaka, kiasi cha kujiamria asili yake; kutaka kuwa na ndoa za watu wa jinsia moja, kinyume cha utu, heshima na misingi bora ya ndoa na familia. Zote hizi anasema Kardinali Sarah ni dalili za kumong'onyoka kwa maadili na utu wema! Mlengwa mkubwa ni binadamu na utu wake.

Licha ya Mama Kanisa kuendelea kushirikiana na wadau mbali mbali katika huduma na maendeleo endelevu ya mwanadamu, anapenda kuchangia kwa namna ya pekee, uelewa wa binadamu mintarafu Maandiko Matakatifu; mwanadamu ambaye yuko wazi mbele ya Mwenyezi Mungu na tayari kusaidiana na jirani zake; akisimama kidete kulinda na kutetea haki zake msingi; akishirikiana na wengine katika huduma ya upendo inayoongozwa na kanuni auni; kwa kutambua tofauti na umuhimu wa jinsia zote mbili kukamilishana. Ikumbukwe kwamba, huduma kwa binadamu ni sehemu ya vinasaba na asili ya Kanisa, kama anavyobainisha Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita.

Huduma kwa watu wanaokabiliwa na dharura zimlenge mtu mzima: kiroho na kimwili; zisiwe ni sababu ya kumdharirisha na kumtweza. Athari za myumbo wa uchumi, kinzani za kisiasa na kijamii sanjari na mmong'onyoko wa maadili na utu wema, yasibezwe na Mashirika ya Misaada ya Kimataifa yakadhani kwamba, yanalo jukumu moja tu la kupambana na baa la njaa na umaskini.

Mwanadamu katika ulimwengu mamboleo na maendeleo ya sayansi na teknolojia ana kiu kubwa ya uwepo wa Mungu katika maisha yake; tabia ya ukanimungu na mawazo mepesi mepesi, kumepelekea taabu na mateso makubwa kwa watu wengi duniani. Kutokana na changamoto hizi, Kanisa bado lina dhamana ya kuendelea kutekeleza utume wake wa Uinjilishaji Mpya, uliovaliwa njuga na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.All the contents on this site are copyrighted ©.