2013-01-16 10:25:26

Vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Jamhuri ya Afrika ya kati inazidi kupamba moto! Watu wasiokuwa na hatia wanapoteza maisha!


Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Afrika ya Kati, linawataka waasi kusitisha mashambulizi dhidi ya watu wasiokuwa na hatia na kufungua milango itakayosaidia Mashirika ya misaada kutoa huduma kwa maelfu ya watu wanaokimbia kutoka nchini humo kutafuta hifadhi na usalama wa maisha yao.

Maaskofu wanaunga mkono ombi lililotolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, akiwataka wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kurudisha tena amani na utulivu nchini humo, kwa kujikita katika majadiliano ya kweli na kina, ili kupata ufumbuzi wa kinzani na mgogoro wa kivita unaoendelea nchini humo. Hadi sasa kuna maelfu ya watu ambao wamepoteza maisha yao na wengine wengi hawana mahali pa kuishi na kwamba, wanahitaji msaada wa dharura.

Maaskofu wanabainisha kwamba, kila siku hali inaendelea kuwa mbaya nchini humo na matumaini ya kupata ufumbuzi wa mgogoro huu wa kivita yanaendelea kufifia siku hadi siku. Vikosi vya waasi wanamtaka Rais Francois Bozize kutoka madarakani.

Maaskofu wanaitaka Serikali iendelee kuwalinda wananchi na vikosi vya majeshi ya uasi kusitisha mashambulizi na kuanza mchakato wa kutafuta suluhu ya amani. Jumuiya ya Kimataifa iendelee kuimarisha ulinzi na usalama wa raia nchini humo.







All the contents on this site are copyrighted ©.