2013-01-16 07:59:26

Mshikamano wa Kanisa Katoliki na watu waliokumbwa na majanga mbali mbali duniani!


Hata katika mapambazuko ya Mwaka Mpya wa 2013 bado habari za vita, kinzani na migogoro ya kisiasa, kijamii na kiuchumi, inaendelea kutawala katika vyombo vya habari kimataifa na kitaifa. RealAudioMP3

Bado kuna umati mkubwa wa watu wanaokabiliwa na baa la njaa, magonjwa na umaskini. Mateso haya yanakolezwa zaidi na athari za myumbo wa uchumi kimataifa pamoja na maafa asilia ambayo yameendelea kutikisa sehemu mbali mbali za dunia.

Askofu mkuu Giampietro Dal Toso, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum anajaribu kupembua kwa kina na mapana shughuli za Baraza hili katika Kipindi cha Mwaka 2012. Anasema, Syria, Libia, Bangaladesh, Sudan ya Kusini, Bolivia na Paraguay ni kati ya nchi ambazo zimenufaika na msaada wa kutoka Cor Unum kwa Mwaka 2012.

Itakumbukwa kwamba, huu ulikuwa ni Mwaka ambao kumefanyika mabadiliko makubwa katika Katiba ya Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, ili kuliwezesha Kanisa kutekeleza kwa umakini mkubwa dhamana na utume wake wa huduma ya upendo kwa wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Ikumbukwe kuwa, huduma ya upendo ni asili ya Kanisa. Ndiyo maana Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, hivi karibuni alichapisha Hati maalum inayoonesha utashi wake kuhusu huduma ya upendo inayotolewa na Kanisa Katoliki, kwa kutoa mwanya kwa waamini kushiriki kikamilifu katika kuwahudumia ndugu zao wahitaji kwa kuzingatia sheria na kanuni za Kanisa, daima wakijitahidi kuonesha mshikamano wa dhati na Askofu mahalia. Huyu ndiye mwenye dhamana ya huduma ya upendo inayotolewa na Kanisa mahalia.

Askofu mkuu Dal Toso anasema kwa masikitiko makubwa kwamba, Mwaka 2012, uliotoweka hivi punde, umekuwa ni mwaka ambao umebeba mateso na mahangaiko makubwa ya watu wa pande mbali mbali za dunia; matajiri kwa maskini, kila mtu ameguswa na kutikiswa na myumbo wa uchumi kimataifa pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi, bila kusahau vita, kinzani na migogoro ya kisiasa, kidini na kijamii inayoendelea kusikika sehemu mbali mbali za dunia, kama Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, alivyobainisha wakati akizungumza na Mabalozi pamoja na Wawakilishi wa nchi na Mashirika ya Kimataifa, mjini Vatican.

Cor Unum ambalo ni Baraza linaloonesha huduma ya ukarimu, upendo na mshikamano kutoka kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kwa kushirikiana na wadau mbali mbali, limeendelea kutoa msaada kwa wakimbizi, watu wasiokuwa na makazi; waathirika wa vita na majanga asilia. Syria ni taifa ambalo limeguswa kwa namna ya pekee na vita inayoendelea kupamba moto siku hadi siku, huku wananchi wasiokuwa na hatia wakiendelea kupoteza maisha na mali yao.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kwa kuguswa na hali ya mateso na mahangaiko ya wananchi wa Syria, mwezi Machi, 2012, alituma msaada maalum kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi, wapatao millioni moja na nusu. Inasikitisha, lakini huu ndio ukweli halisi.

Hali ilivyozidi kuchafuka, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, alimtuma Kardinali Robert Sarah, Rais wa Baraza la Kipapa la Cor Unum, hapo Mwezi Novemba, 2012, nchini Lebanon, ili kutoa mchango wake wa pekee kama alama ya mshikamano wa Kanisa na wote waliokuwa wanateseka kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.

Huu ulikuwa ni mchango uliotolewa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya iliyokuwa inafanyika hapa mjini Vatican, Mwezi Oktoba, 2012. Mababa wa Sinodi walikuwa wameonesha nia ya kwenda wao wenyewe nchini Syria ili kuwasilisha mchango wao, lakini kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wao, wakashindwa kutekeleza nia hii njema.

Hadi sasa kuna jumla ya Mashirika 25 ya Misaada ya Kanisa Katoliki yanayotekeleza huduma ya upendo kwa wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum kutoka Syria. Mashirika haya yanatoa msaada wake moja kwa moja nchini Syria ili kuziwezesha familia kupata walau mahitaji ya msingi, huduma inayotolewa kwa upendo mkubwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa nchini Syria. Sehemu ya pili ya msaada huu, inatolewa kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria wanaoishi nchini Lebanon, Jordani, Iraq na Uturuki. Hapa hata Mashirika ya Misaada Kimataifa yanajihusisha kikamilifu.

Jumla ya dolla za Kimarekani Millioni moja zilikusanywa ili kusaidia huduma kwa wakimbizi kutoka Syria. Hiki ni kielelezo cha mshikamano wa upendo kutoka kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwamba, msaada huu ulitolewa kwa wote bila ya ubaguzi.

Cor Unum inaendelea pia kufuatilia utekelezaji wa mikakati mbali mbali ya maendeleo kwa ajili ya ujenzi wa Haiti mpya iliyokumbwa na tetemeko la ardhi, kwanza kabisa katika ujenzi wa shule mbili, kwani Kanisa lina amini kwamba, watu wakiwezeshwa katika elimu, wanaweza kujikomboa hata katika medani nyingine za maisha.

Cor Unum inaendelea kusisitiza kwamba, Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki hayana budi kuhakikisha kwamba, yana bana matumizi ya fedha za misaada ili fedha hizi ziweze kuwafikia walengwa zaidi badala ya kuishia mifukoni mwa viongozi na wahudumu wa Mashirika ya Misaada ya Kanisa. Wawajibike na kutoa taarifa rasmi ya mapato na matumizi ya fedha za Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki. Hii ni dhamana nyeti inayowawajibisha kujikita katika misingi ya ukweli na uwazi.

Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum linatarajia kuanza mkutano wake wa Mwaka, hapo tarehe 17 hadi tarehe 19 Januari 2013; likiongozwa na mada “Uelewa wa mwanadamu mintarafu Ukristo na maadili mapya kimataifa”. Ulimwengu wa utandawazi unakabiliwa na changamoto ya kupata mwono halisi wa mwanadamu, jambo ambalo wakati mwingine linasigana na uelewa wa mwanadamu mintarafu Mafundisho ya Kanisa Katoliki, kama alivyobainisha Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, wakati wa salam na matashi mema kwa wasaidizi wake wa karibu, mwishoni mwa Mwezi Desemba 2012.

Uelewa na mwono wa mwanadamu mintarafu ufunuo wa Maandiko Matakatifu ni utajiri na urithi mkubwa kwa watu wanaoishi katika ulimwengu mamboleo. Cor Unum inapenda kuhamasisha mwono huu katika huduma mbali mbali zinazotolewa kwa binadamu sehemu mbali mbali za dunia.

Askofu mkuu Giampietro Dal Toso, Katibu mkuu wa Cor Unum anasema lengo ni kumtambua mtu, lengo la huduma na mchango wa Kanisa Katoliki kama utakavyopembuliwa na wasomi katika mkutano maalum utakaofanyika kati ya tarehe 4 hadi tarehe 5 Machi 2013. Kanisa Katoliki nchini Ujerumani wana uzoefu na mang’amuzi mapana zaidi katika sekta hii.

Itakuwa ni fursa ya kujifunza kwa kina juu ya Taalimungu ya Upendo na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Hizi ni kati ya changamoto ambazo zinaendelea kutolewa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika Waraka wake wa kichungaji, Ukweli katika Upendo na Mungu ni Upendo. Ni wakati wa kujadili pia dhana na utume wa Kanisa katika Jamii. Kwa ufupi huu ndio utekelezaji wa malengo na mikakati ya Baraza la Kipapa linaloratibu Misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum pamoja na shughuli wanazotarajia kuzitekeleza kwa siku za usoni.
All the contents on this site are copyrighted ©.