2013-01-16 09:24:33

Matumaini ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 huko Rio De Janeiro


Katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 huko Rio de Janeiro kuanzia tarehe 23 hadi 28 Julai 2013, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anatarajiwa pia kupata fursa ya kujionea mwenyewe mandhari ya mji wa Rio de Janeiro, wakati atakapokuwa anazungushwa na Helikopta.

Hayo yamesemwa na Askofu mkuu Oran Joao Tempesta wa Jimbo kuu la Rio de Janeiro ambaye yuko hapa mjini Vatican hadi hapo tarehe 25 Januari, 2013 kushiriki katika vikao mbali mbali na Mabaraza ya Kipapa kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013, ambayo Kanisa Katoliki Brazil ni mwenyeji wake.

Inakadiriwa kwamba, vijana zaidi ya millioni mbili kutoka sehemu mbali mbali za dunia watashiriki katika kilele cha maadhimisho haya. Vijana watakuwa na fursa ya kufanya Njia ya Msalaba ambayo imekuwa na mvuto mkubwa katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa, kama kielelezo cha ushuhuda wa Imani yao kwa Kristo, aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka wafu, ili kuwakirimia waja wake maisha ya uzima wa milele. Njia ya Msalaba itafanyika kwenye Fukwe maarufu za Copacabana, Brazil.

Kamati ya Maandalizi kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil inaendelea kushirikiana na Mabaraza na vitengo mbali mbali vinavyohusiana na hija za kichungaji za Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili kukamilisha mambo yote kwa wakati muafaka. Maandalizi haya yanawashirikisha pia viongozi mahalia kutoka Brazil kwani hata wao watakuwa nafasi ya pekee katika hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, nchini Brazil.

Itakumbukwa kwamba, Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yanasimamiwa na kuendeshwa na Baraza la Kipapa la Walei. Katika Liturujia ambamo Baba Mtakatifu anatarajiwa kushiriki, Mshereheshaji Mkuu wa Kipapa anahusika moja kwa moja, bila kusahau mawasiliano, ulinzi na usalama.

Baba Mtakatifu anatembelea Brazil si tu kama mkuu wa Nchi ya Vatican, bali pia kama Khalifa wa Mtakatifu Petro anayekwenda kuwaimarisha ndugu zake katika Imani na kuwapatia vijana matumaini mapya ya kuendelea kuwa ni wadau wakuu katika azma ya Uinjilishaji Mpya, changamoto inayofanyiwa kazi na Mama Kanisa wakati huu.







All the contents on this site are copyrighted ©.