2013-01-16 08:20:29

Katekesi ya kina na makini, iwasaidie waamini kukumbatia Fumbo la Msalaba linaloonesha ushindi wa Kristo!


Askofu Damian Dallu wa Jimbo Katoliki Geita, Tanzania, katika mahojiano maalum na Radio Vatican, katika maadhimisho ya Mwaka wa Imani, anawaalika waamini na vyama vya kitume kuhakikisha kwamba, wanatumia fursa hizi kwa ajili ya kuimarisha imani yao inayopata chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu, Katekesimu Mpya ya Kanisa Katoliki, Mafundisho Jamii ya Kanisa na bila kusahau Mapokeo hai ya Mama Kanisa. RealAudioMP3

Anasema, Katekesi ya kina na makini kwa waamini inalenga kuwapatia waamini hao, mafundisho ya kina kuhusu: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha Adili pamoja na Maisha ya Sala. Kwa njia hii, waamini wataweza kuwa na msimamo thabiti wa imani yao kwa Kristo aliyezaliwa, akateswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Katekesi ya kina inamchangamotisha mwamini kutekeleza majukumu yake ya kuyatakatifuza malimwengu, kwa kuendelea kukumbatia Fumbo la Msalaba, ambalo leo hii, limekuwa ni tishio kwa watu wengi, kwani wanataka kuukimbia ukweli kuhusu Msalaba katika uhalisia wa maisha yao na kutaka maisha ya mkato ambayo kimsingi hayapo katika hija ya maisha ya mwanadamu. Watu katika ulimwengu mamboleo wanataka kumwona Yesu mwenye mali anayejibu sala zao kila wakati "wanapombeep" au wanapokumbana na ukata kana kwamba amekuwa ni "Banckomat".

Askofu Dallu anasema kwamba, Fumbo la Umwilisho linaloonesha unyenyekevu wa Mwana wa Mungu linapata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaami: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, kielelezo cha ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Bila Katekesi makini, waamini watakuwa na Yesu bandia, aliye nje ya imani na mafundisho ya Kanisa.

Kumbe, Neno la Mungu, Katekesim u Mpya ya Kanisa Katoliki, Mafundisho Jamii ya Kanisa na Mapokeo Hai ya Kanisa ziwe ni nyenzo msingi za kuifahamu, kuiungama na kuitolea ushuhuda imani kwa Kristo na Kanisa lake.







All the contents on this site are copyrighted ©.