2013-01-16 10:39:09

Ibueni mbinu mkakati wa kukabiliana na uhaba wa fursa za ajira, kuepukana vifo vya vijana wengi!


Kardinali Anthony Olubumni Okodgie, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Lagos, Nigeria, anasema amesikitishwa na vitendo vya hujuma vinavyofanywa kwenye Bomba la mafuta na watu wasiopenda maendeleo nchini Nigeria, kiasi hata cha kupelekea vijana wengi kuendelea kupoteza maisha yao kutokana na kulipukiwa na mafuta.

Hii ni changamoto kwa viongozi wa Serikali na wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanaibua mbinu mkakati utakaowapatia vijana fursa za ajira kwani wizi na hujuma zinazofanywa kwenye Bomba la Mafuta ni matokeo ya umati mkubwa wa vijana kukosa fursa za ajira nchini humo.

Vijana wakati wakigombania kupata nafasi ya kuchota mafuta, walijikuta wanatupiwa risasi na walinzi wa Bomba la Mafuta, jambo ambalo lingeweza kuepukwa ili kuokoa maisha ya watu. Vijana wengine nchini Nigeria wanaonekana kwamba, wamechanganyikiwa kutokana na ukweli kwamba, wengi wao hawana fursa za ajira na matokeo yake, wamejikuta wakijiingiza katika vitendo vinavyopelekea uvunjifu wa amani na usalama kwa raia na mali zao.







All the contents on this site are copyrighted ©.