2013-01-15 07:57:58

Sheria ya nchi isikumbatie utamaduni wa kifo kwa kisingizio cha kuokoa maisha ya Mamamjamzito!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland linabainisha kwamba, maisha ya Mama na Mtoto ambaye yuko bado tumboni ni matakatifu na yanapaswa kutunzwa na kuheshimiwa kikatiba na kamwe, sheria za nchi zisikumbatie utamaduni wa kifo, kwa kisingizio cha kuokoa maisha ya Mama mjamzito peke yake. Katiba ya Ireland inakataza utoaji mimba kwa hiyari, lakini inaruhusu mimba hiyo itolewe ikiwa kama maisha ya Mamamjamzito yako hatarini.

Kuna matukio kadhaa ambayo yameendelea kutokea nchini Ireland kiasi cha kuwafanya Maaskofu Katoliki kuibua tena mjadala wa sheria ambayo itaheshimu zawadi ya maisha ya Mama na Mtoto ambaye bado yuko tumboni, kwani hii ni sehemu ya haki msingi wa binadamu. Askofu Christopher Jones, Mwenyekiti wa Tume ya Ndoa na Familia, Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland anasema kwamba, utoaji wa mimba ni mauaji ambayo kamwe hayawezi kuhalalishwa kisheria na ni kinyume cha maadili na utu wema.

Kutokana na kushamiri kwa utamaduni wa kifo, baadhi ya wahudumu wa sekta ya afya wamejikuta wakishinikizwa kutoa mimba kwa kisingizio cha kutaka kuokoa maisha ya Mamamjamzito. Madaktari wanapaswa kutambua kwamba, wao ni wadau wakuu wa maisha, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kuokoa maisha ya mama na mtoto ambaye bado yuko tumboni mwa mama yake, kwani maisha ya watu hawa ni matakatifu, yanapaswa kuheshimiwa na kulindwa kikatiba.

Majadiliano yote haya hayana budi kutoa kipaumbele cha pekee kwa wanawake, kwa kuwaelewa, kuwahurumia na kuwaheshimu katika shida na mahangaiko yao ya ndani. Hakuna sababu za msingi zinazoweza kupelekea watu kutaka kukumbatia utamaduni wa kifo. Wananchi wa Ireland wanataka sasa Serikali iitishe kura ya maoni ili kutengua sheria inayoruhusu utoaji mimba kwa kisingizio cha kutaka kuokoa maisha ya mamamjamzito. Inasikitisha kuona kwamba, kuna zaidi ya wanawake elfu nne kutoka Ireland wanaojihusisha na suala la utoaji mimba nje ya nchi yao.All the contents on this site are copyrighted ©.