2013-01-15 09:26:47

Mapinduzi ya Zanzibar 1964 yalipania kungo'a ukandamizaji, unyonyaji na ubaguzi


Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania amesema kuwa moja ya faida kubwa na nyingi za Mapinduzi ya Zanzibar ni kufunguliwa kwa namna kubwa sana kwa nafasi na fursa za elimu kwa watoto wa Wazanzibari Wazawa. Sababu kubwa ya Chama cha Afro- Shiraz Party kufanya Mapinduzi ya mwaka 1964 ilikuwa ni kuondoa ukandamizaji, unyonyaji na ubaguzi waliokuwa wanafanyiwa Zanzibari Wazawa katika kupata huduma ikiwepo elimu.

Akizungumza, Jumamosi, Januari 12, 2013, wakati anazindua Shule ya Sekondari ya Mlimani-Matemwe, Mkoa wa Kaskazini, kwenye pwani ya kaskazini ya Kisiwa cha Unguja, Rais Kikwete amesema kuwa inashangaza sana kuwa baadhi ya watu wanaweza kuendelea kuyabeza Mapinduzi ya Zanzibar wakati yameleta faida kubwa na nyingi kwa wananchi na wanazijua. “Sote tunatambua sababu kubwa ya Chama cha ASP kufanya Mapinduzi ya mwaka 1964 ilikuwa ni kuondosha ukandamizaji, unyonyaji na ubaguzi waliokuwa wanafanyiwa Wazanzibari wazawa katika kupata huduma muhimu ikiwepo elimu. Idadi ya skuli ilikuwa ndogo sana na kwa makusudi wazawa wenzetu chache ndio walibahati kupata elimu,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Baada ya Mapinduzi, skuli nyingi zilijengwa na vijana wengi zaidi wanapata elimu. Kazi hiyo inaendelea kama tunavyoshuhudia leo.” Rais Kikwete aliongeza: “Zanzibar na Pemba zilikuwa na shule tatu tu za sekondari za Serikali kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964 – moja ilikuwa Pemba ikiitwa Saidi Abdallah Secondary School na mbili zilikuwa Zanzibar, basi. Zilizobakia zilikuwa shule za sekondari za dini. Leo tu, tunafungua kwa mpigo shule 21 za sekondari mpya. Moja hii ambayo ni moja ya shule 13 ambazo ujenzi wake umekamilika. Nyingine nane zikiwa zinajengwa ikiwa ni pamoja na chuo kipya cha ualimu cha Benjamin William Mkapa.”

Uzinduzi wa shule hiyo yenye majengo na huduma za kisasa ikiwa ni pamoja na maabara za masomo ya fikizia, kemia, biolojia na kompyuta ni sehemu ya Sherehe za Miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambayo sherehe zake zimefanyika leo kwenye Uwanja wa Amaan, mjini Zanzibar, na kuhudhuriwa na Rais kikwete. Shule hiyo iliyogharimu kiasi cha Sh. Bilioni 1.8 mpaka sasa ni moja ya shule 19 za sekondari zinazojengwa Tanzania Visiwani chini ya Mradi wa Uimarishaji wa Elimu ya Lazima (ZABEIP) miaka mitano unaogharimiwa kwa pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya Dunia.

Serikali ya Mapinduzi (SMZ) inatoa dola za Marekani milioni sita na Benki ya Dunia dola za Marekani milioni 42 ikiwa ni mkopo wenye masharti nafuu na mradi wenyewe ulioanza kutekelezwa Julai 2008 unafikia mwisho wake Juni mwaka huu, 2013. Chini ya mradi huo, zinajengwa shule 10 za sekondari (kidato cha kwanza hadi cha sita) katika kila wilaya za Tanzania Visiwani, zinajengwa shule tisa za sekondari (kidato cha kwanza hadi cha nne) – tano Unguja na nne kisiwani Pemba, kinajengwa chuo kipya cha ualimu cha William Benjamin Mkapa Kisiwani Pemba na shule sita zinafanyiwa matengenezo makubwa.

Mradi huo pia ni matokeo ya mazungumzo kati ya Rais Kikwete na uongozi wa Benki ya Dunia wakati alipofanya ziara yake ya kwanza Marekani mwaka 2006 baada ya kuwa amekuwa Rais wa Tanzania ambako aliushawishi uongozi wa Benki hiyo kukubali kutoa fedha za kugharimia mradi huo mkubwa zaidi kuliko mwingine wowote kufanywa na Serikali katika historia ya Zanzibar. Aidha, kutekelezwa kwa mradi huo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa Uchaguzi Mkuu wa 2010 ambayo iliiagiza Serikali ya Mapinduzi kujenga shule za kisasa za sekondari 21 katika wilaya zote za Unguja na Pemba.

Chini ya Mradi wa ZABEIP, tayari shule za sekondari 13 zimekamilika kujengwa na ujenzi wa shule sita zilizobakia pamoja na Chuo cha Ualimu cha Benjamin William Mkapa Kisiwani Pemba unaendelea. Na ili kufikisha idadi ya shule 21 za sekondari kama inavyoelekeza Ilani ya CCM, ujenzi wa shule nyingine mbili zilizosalia unaendelea katika eneo la Mkanyageni Kisiwani Pemba na Kiblateni Kisiwani Unguja kwa gharama ya pamoja ya Serikali ya Mapinduzi na Benki ya Kiarabu ya Maendeleo (BADEA).

Shule ya Mlimani-Matemwe yenye huduma kamili za elimu na ambayo ni sekondari ya kidato cha kwanza hadi cha nne, ilianza kupokea wanafunzi Septemba mwaka jana kwa vidato vya kwanza na tatu. Wanafunzi 231 ndiyo walianzisha shule hiyo ya kutwa na yenye hadhi ya wilaya ikiwa na wavulana 145 na wasichana 86. Shule hiyo ina walimu tisa wakiwemo wawili wa kujitolea kutoka Nigeria. Sherehe hizo za uzinduzi wa shule hiyo zilizohudhuriwa na viongozi wa SMZ akiwamo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Idi imehudhuriwa na mamia ya wakazi wa eneo la Mlimani-Matemwe.
All the contents on this site are copyrighted ©.