2013-01-15 10:33:29

Mafundisho Jamii ya Kanisa yanagusa undani wa maisha na utume wa Kanisa katika huduma


Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani, hivi karibuni ameshiriki katika Kongamano la Kimataifa lililoandaliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Gabon kuhusu masuala ya haki na amani, mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Anasema, Kanisa limeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha, kufundisha na kutetea haki na amani, kama sehemu ya mchakato wa utume na maisha yake hapa duniani.

Kwa hakika, Kanisa limekuwa ni mwanga wa mataifa kuhusiana na masuala ya haki na amani katika masuala yanayogusa uchumi na haki jamii. Anasema, Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapata chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu na kufafanuliwa kwa kina katika maisha na utume wa Yesu; dhamana inayoendelezwa na Mama Kanisa, sehemu mbali mbali za dunia. Ndiyo maana Kanisa limekuwa ni mdau wa pekee katika kuwahudumia na kuwatetea wakimbizi, wahamiaji, wagonjwa, wasafiri; watoto yatima, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana na hali yao ya maisha.

Dhamana hii inatekelezwa na Mama Kanisa kwa njia ya Mashirika mbali mbali ya Kitawa na Kazi za Kimissionari, kama kielelezo cha mshikamano wa upendo unaojionesha katika Nyaraka mbali mbali za Kanisa; na Muhtasari wake unapatikana katika Mafundisho Jamii ya Kanisa, ambayo wengine wanayaita Biblia ya Waamini Walei, katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Ni nyaraka zilizotolewa kuanzia kwa Papa Leo wa Kumi na tatu hadi wakati huu, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika waraka wake wa kichungaji, Upendo katika Ukweli, uliotolewa kunako mwaka 2007.

Kardinali Turkson anasema kwamba, chimbuko na historia ya Mafundisho Jamii ya Kanisa ni: utu na heshima ya mwanadamu; haki, amani, ustawi na maendeleo ya mwanadamu kiroho na kimwili. Mafundisho Jamii ya Kanisa ni jibu makini kutokana na mahangaiko ya mwanadamu wakati wa Mapinduzi ya Viwanda Barani Ulaya na madhara yake yakajionesha katika maisha ya watu waliojikuta wakinyanyasika na kudhulumiwa, kiasi kwamba, haki zao msingi ziliwekwa rehani.

Mfumo wa uchumi wa kikomunisti na Kibepari, ukaibua pia changamoto mbali mbali, kiasi hata cha kujikuta dunia imegawanyika katika makundi: Nchi zilizozoendelea, nchi zinazoendelea na nchi za dunia ya tatu. Huko ndiko zinakopatikana nchi zilizoko Afrika na Asia, ambazo pia zilionja makucha ya utawala wa kikoloni. Kuanguka kwa Ukuta wa Berlini na kuhitimishwa kwa vita baridi kati ya Marekani na Russia; na matokeo yake yakawa ni mageuzi makubwa katika: uchumi, siasa na Jamii.

Kwa sasa Ulimwengu wa utandawazi unashuhudia mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia; kukwama kwa juhudi za maendeleo pamoja na athari za myumbo wa uchumi kimataifa; athari za mabadiliko ya tabia nchi bila kusahau kumong'onyoka kwa maadili na utu wema. Zote hizi ni changamoto zinazofanyiwa kazi na Mama Kanisa katika Mafundisho Jamii, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na maendeleo yake: kiroho na kimwili; utu na heshima yake, kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Lengo la Mafundisho Jamii ya Kanisa ni kujenga mji wa Mungu hapa duniani, kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha: upendo, haki, amani na mafao ya wengi na wala si kwa ajili ya kikundi cha watu wachache ndani ya Jamii.All the contents on this site are copyrighted ©.