Maelfu ya watu wajimwaga barabarani kutetea msingi bora wa ndoa na familia!
Takribani watu millioni moja kutoka sehemu mbali mbali za Ufaransa, Jumapili, tarehe
13 Januari 2013 walifanya maandamano makubwa kupinga muswada wa sheria unaotaka kuruhusu
watu wa jinsia moja kuoana kama Bwana na Bibi na hivyo pia kuruhusia kuasi watoto.
Umati huu wa watu ulikusanyika kama kielelezo cha Jamii inayothamini na kuenzi tunu
msingi za maisha ya ndoa na familia, inayojengeka katika uhusiano wa dhati na unaowajibisha
kati ya Bwana na Bibi.
Watu wanasema wanaunga mkono ndoa asilia inayoundwa
kati ya Bwana na Bibi, ndiyo maana wamejitokeza kwa wingi kupinga vitendo vinavyokiuka
utu na heshima ya binadamu kwa kisingizio cha uhuru na haki sawa. Haya ni maandamano
yaliyowashirikisha watu kutoka dini na madhehebu mbali mbali, wote wakiwa na lengo
la kusimama kidete kutetea misingi bora ya ndoa na familia, dhidi ya mmong'onyoko
wa maadili na utu wema, unaoendelea kujitokeza kwa mwamvuli wa uhuru na haki msingi
za binadamu.
Wananchi wa Ufaransa wanabainisha kwamba, Serikali inapaswa kuwa
makini katika masuala yanayogusa: Ndoa na Familia; Haki Msingi za Watoto pamoja na
kujenga utamaduni wa upatanisho wa kitaifa, ili wananchi waweze kuendelea kuishi kwa
amani na utulivu.