2013-01-15 08:55:18

Maadhimisho ya Jubilee ya miaka 100 ya Seminari Kuu ya Katigondo, Uganda yaanza kupamba moto!


Seminari kuu ya Katigondo inayomilikiwa na kuendeshwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda, inajiandaa kuadhimisha Jubilee ya Miaka 100 tangu ilipoanzishwa katika eneo la Afrika Mashariki. Seminari hii ambayo imejengwa katika Jimbo Katoliki Masaka, Uganda ni utajiri na urithi mkubwa wa Kanisa Katoliki si tu nchini Uganda bali katika nchi za Afrika Mashariki na Kati, ambazo kwa sasa zinaunda AMECEA, kwani wengi wa viongozi wake walipata majiundo yao kwenye Seminari kuu ya Katigondo.

Kutokana na ukubwa wa tukio hili la kihistoria, Askofu John Baptist Kagwa wa Jimbo Katoliki Masaka, Uganda, anawaalika watu wote wenye mapenzi mema kutoka ndani na nje ya Uganda, kuchangia kwa hali na mali, ili kufanikisha Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Seminari kuu ya Katigondo, Uganda. Walengwa wakuu ni wanafunzi wote waliobahatika kupata majiundo yao Seminarini hapo. Lengo ni kuweza walau kukusanya kiasi cha shilingi za Uganda billioni 53 sawa na kiasi cha Euro millioni 15.

Mapadre kutoka Uganda, tayari wamekwisha changia sehemu ya fedha hii. Katika kipindi cha Miaka 100 iliypita, Seminari kuu ya Katigondo imebahatika kutoa majiundo makini kwa Majandokasisi elfu nne; kati yao waliobahatika kufikia Daraja takatifu la Upadre ni 1,700 na kati ya Mapadre hawa kuna Maaskofu 27. Seminari hii ilijengwa ili kutoa huduma kwa Majandokasisi 150, kwa sasa kuna jumla ya Mafrateri 270 wanaojiandaa kwa ajili ya maisha na utume wa Kipadre kwa kujikita katika: Masomo, Sala, Maisha ya Kijumuiya na Elimu ya Kujitegemea, hasa katika shughuli za kilimo na ufugaji.All the contents on this site are copyrighted ©.