2013-01-15 07:27:26

Huduma ya upendo ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita ameelezea nia yake binafsi inayoonesha kwamba huduma ya upendo ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa. Mama Kanisa anatekeleza wajibu na utume wake kwa kuzingatia misingi mikuu mitatu: Kutangaza Neno la Mungu; kuadhimisha Sakramenti za Kanisa na huduma. Mambo haya matatu yanakwenda pamoja na kamwe hayawezi kutenganishwa. RealAudioMP3

Huduma ya upendo ni alama makini ya utume wa Kanisa na utambulisho wake. Kumbe, waamini wote wanawajibu wa kutekeleza katika maisha yao amri ya upendo ambayo Yesu mwenyewe amewaachia wafuasi wake; kwa kuwasaidia watu katika mahitaji yao ya kimwili na kiroho.

Kanisa katika ujumla wake anasema Baba Mtakatifu, linatakiwa kutekeleza huduma ya upendo kuanzia katika Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo, kwenye Makanisa mahalia hadi kufikia ngazi ya Kanisa la Kiulimwengu. Hali hii inahitaji kwa namna ya pekee uratibu wa shughuli hizi kwa ajili ya Jumuiya, kwa kuwa na taasisi ambayo itaratibu mikakati yote.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anabainisha kwamba, katika Waraka wake wa kichungaji, Mungu ni Upendo, alielezea kuwa, kadiri ya mpango wa Kanisa unaosimikwa kwa Maaskofu ambao ni waandamizi wa Mitume, wanao wajibu wa kutekeleza huduma ya upendo katika Majimbo yao mintarafu Sheria za Kanisa, ambamo kunapembuliwa kwa mapana utume wa Askofu mahalia.

Maaskofu wanao wajibu mkubwa kwa Kanisa zima kuhakikisha kuwa, wanatekeleza asili ya Kanisa katika utoaji wa huduma ya upendo kadiri ya dhamana na wajibu wa Askofu mahalia, kwa kuzingatia sheria hasa pale anapotekeleza wajibu huu kwa kuungana na Maaskofu wengine.

Baba Mtakatifu kwa waraka huu anapenda kutangaza rasmi nia yake inayotoa mwelekeo wa kisheria utakaoratibu shughuli zote za huduma ya upendo zinazotolewa na kikanisa ambazo ziko karibu na asili ya Kanisa katika kuhudumia pamoja na utume wa Kiaskofu. Huduma ya upendo haitaweza kuzaa matunda yanayokusudiwa ikiwa kama hailengi kuonesha upendo kwa binadamu, upendo unaorutubishwa kwa kukutana na Kristo.

Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki yanayojihusisha na matendo ya huruma, yasijikite tu katika kutafuta na kugawa fedha kwa ajili ya huduma, bali yaguswe na mahitaji ya watu kwa kuwamasisha waamini kutambua umuhimu wa kushirikishana, kuheshimiana na kupendana mintarafu moyo wa Injili ya Kristo.

Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki yajitofautishe na mashirika mengine ya misaada ya kijamii kwa kuwa makini na huduma wanaozotoa kwa wahitaji na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Huduma hizi zinaweza kuwa ni katika ngazi ya Kiparokia, Kijimbo, Kitaifa na Kimataifa. Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki, Caritas ni mali ya Kanisa na limepata mafanikio makubwa, linaheshimiwa na kuthaminiwa na waamini pamoja na watu wengine sehemu mbali mbali za dunia kutokana na ukarimu kama kielelezo makini cha imani kwa kujibu kwa wakati muafaka mahitaji ya maskini.

Kutokana na mwelekeo kama huu, waamini wengi wameanzisha Mashirika ya misaada ambayo ni kielelezo cha huduma ya upendo kwa wahitaji. Mashirika haya yanatofautiana katika asili na sharia, ingawa yanaoneshwa jinsi ambavyo yanahitaji kujibu kilio cha huduma ya upendo kwa wahitaji.

Baba Mtakatifu anasema Mashirika haya hayana budi kuratibiwa na Kanisa kama kielelezo cha viongozi wa Kanisa kutambua na kuthamini mchango wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kuheshimu sheria na kanuni husika, uongozi uliopo kama kielelezo cha uhuru wa Wabatizwa. Itakumbukwa kwamba, Kanisa Katoliki lina taasisi zake linaloratibu misaada inayokusanywa kutoka kwa waamini mbali mbali; taasisi hizi zinafuata sheria na uongozi unaoziwezesha kujibu kwa uhakika mahitaji ya watu.

Baba Mtakatifu anasema, Mashirika yote haya katika utekelezaji wa majukumu yake, hayana budi kufuata Mafundisho ya Kanisa, Nia ya wahisani pamoja na kuzingatia sheria za nchi pamoja na Sheria za Kanisa kutokana na wajibu ambao wahusika wanajitwalia, licha ya kuonesha tofauti mbali mbali. Sheria zinahitajika kama sehemu ya utekelezaji wa haki na dhamana ya Maaskofu mahalia kwa waamini wao kwa kuheshimu uhuru wa kila taasisi.
All the contents on this site are copyrighted ©.