2013-01-14 14:39:12

Wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican wanahimizwa kutolea ushuhuda ujumbe wa Injili katika medani mbali mbali za maisha!


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumatatu, tarehe 14 Januari 2013 amekutana na kuzungumza na wanajenzi wa vikosi vya ulinzi na usalama vinavyotekeleza majukumu yao mjini Vatican, kama sehemu ya utamaduni wa kutakiana kheri na matashi mema kwa Mwaka Mpya wa 2013.

Amewashukuru kwa utekelezaji wa majukumu ya ulinzi na usalama mjini Vatican yanayozingatia sadaka na weledi wa kazi, kwa maelfu ya watu wanaofika mjini Vatican kumtembelea Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na Makaburi ya Mitume na Mapapa waliotanguliwa mbele ya haki wakiwa na tumaini la ufufuko, lakini kwa namna ya pekee Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili.

Utekelezaji wa majukumu haya unajionesha hata wakati wa hija zake za kichungaji ndani na nje ya mji wa Roma, mambo yanayomsukuma Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kuonesha kweli moyo wa shukrani kutokana na utayari wao katika huduma, makini na watu ambao wana sifa. Hii ni heshima kama sehemu ya utambulisho wao kama wafanyakazi wa serikali na Wanajumuiya wa Kanisa na ni kielelezo cha uhusiano mwema kati ya Vatican na Serikali ya Italia.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, magumu na sadaka kubwa wanayoitoa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, bila kusahau changamoto na hatari wanazoweza kukutana nazo, kiwe ni kielelezo cha imani yao ya Kikristo, tunu msingi ya maisha ya kiroho ambayo wao wameirithi kutoka kwa wazazi wao na sasa wanaalikwa kuwarithisha pia watoto wao.

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani iwe ni fursa kwa wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama kutangaza kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, Ujumbe wa Injili ya Kristo uweze kupenya katika dhamiri, maisha ya kawaida kwa kushuhudia nguvu ya upendo wa Mungu katika medani mbali mbali za maisha.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, katika ujumbe wake kwa Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2013, amebainisha aina mbali mbali za kazi za kulinda na kudumisha amani, jambo linaloonesha wito wa mwanadamu katika kulinda amani, kwani hamu ya kuishi katika amani ni kielelezo cha tamaa ya kutaka kupata utimilifu wa maisha na furaha ya kweli.

Baba Mtakatifu anawatakia wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama utaratibu na utulivu; mambo yanayojenga maisha yenye amani na utulivu na kielelezo cha ustaarabu wa kweli. Anawaweka wote chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria, ili aweze kuwaombea kwa Mwanaye Mpendwa: maendeleo, amani, utulivu na kuwalinda dhidi ya hatari zote za maisha: kiroho na kimwili.







All the contents on this site are copyrighted ©.