2013-01-14 10:03:26

Umuhimu wa kuwekeza katika elimu kama njia ya kudumisha misingi ya haki, amani na maendeleo endelevu


Uwekezaji katika sekta ya elimu Barani Afrika, Asia na kwa nchi zilizoko Amerika ya Kusini ni sehemu ya mchakato unaopania kuwajengea wananchi hao uwezo wa kupambana na umaskini na maradhi pamoja na kuunda mfumo wa sheria ulio sawa na unaozingatia utu na heshima ya binadamu. RealAudioMP3
Lengo ni kuhakikisha kwamba haki inatendeka, kwa kuwa na mifumo makini ya uchumi. Haki inaweza kutendeka pale tu watu wenyewe wanatambua na kuheshimu haki msingi. Hivyo basi, ujenzi wa msingi wa haki na amani hauna budi kujielekeza katika kuwaandaa watu kupambana kufa na kupona dhidi ya rushwa, ufisadi na matendo ya jinai; biashara haramu ya dawa za kulevya pamoja na kuondokana na mambo yote ambayo yanaendelea kujenga hofu na migawanyiko mbali mbali ndani ya Jamii, kwani yote haya ni kikwazo cha maendeleo endelevu, amani na utulivu katika Jamii.
Ni changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican, wakati wa salam na matashi mema kwa Mwaka 2013. Anasema, amani inawekwa katika mtihani mkubwa kutokana na mambo ambayo yanaendelea kutishia uhuru wa kidini, jambo ambalo Jumuiya ya Kimataifa haijalipatia umuhimu wa kutosha. Matokeo yake, baadhi ya watu wanakosa uvumilivu na kuanza kushambulia watu, alama za kidini na utambulisho wa Mashirika ya kidini.
Baadhi ya waamini na kwa namna ya pekee, Wakristo hawashirikishwi katika kuchangia mafao ya wengi kwa njia ya taasisi zao za elimu na huduma za kijamii. Ili kulinda na kudumisha uhuru wa kidini anasema Baba Mtakatifu, kuna haja ya kuheshimu dhamiri za watu, kwani unagusa masuala muhimu sana ya kimaadili na kidini yanayofumbatwa katika utu na heshima ya binadamu. Hizi ni nguzo msingi na utambulisho wa taasisi na uhuru wa kidini. Nguzo hizi zisipoheshimiwa na kuthaminiwa, matokeo yake ni watu kushindwa kuvumiliana na amani inaweza kutoweka.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anabainisha kwamba, ujenzi wa amani hauna budi kujikita katika majadiliano pamoja na kujikita katika maboresho ya mahusiano kati ya Serikali na Kanisa. Tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Poland, Patriaki wa Moscow pamoja na Serikali ya Russia na Poland ni mfano wa kuigwa. Kuna mifano mingi ya kuigwa katika majadiliano ya kidini kutoka Mindanao, Ufilippini. Amani inakamilishwa kwa njia ya upendo na haki; mambo ambayo ni msingi wa utume wa kidiplomasia unaotekelezwa na Vatican, sehemu mbali mbali za dunia. Hiki ni kipaumbele cha kwanza cha Kanisa Katoliki, kwani haki na amani ni chanda na pete.
Mama Kanisa anatekeleza wajibu huu kwa njia huduma zinazojionesha kwa namna ya pekee katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu ya Jamii. Kanisa limeendelea kuwasaidia wakimbizi wanaolazimika kuyahama makazi yao kutokana na vita na sasa Kanisa linajielekeza katika kuwahudumia watu waliokumbwa na maafa asilia, sehemu mbali mbali za dunia. Matukio yote haya yajenge na kuimarisha moyo wa upendo na mshikamano unaoongozwa na kanuni auni.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anasema kuwa, imekwisha gota miaka hamsini, tangu Papa Paulo wa Sita, alipowahimiza Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa kweli ni wajenzi wa haki na amani, changamoto endelevu hata kwa Mabalozi na wawakilishi wa nchi na Mashirika ya Kimataifa sehemu mbali mbali za dunia.

All the contents on this site are copyrighted ©.