Ubatizo wa Bwana ni kielelezo cha hali ya juu kabisa ya unyenyekevu unaopata hitimisho
lake katika Fumbo la Pasaka!
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika maadhimisho ya Sherehe za Ubatizo
wa Bwana, Jumapili tarehe 13 Januari 2013, Kwenye Kikanisa na Sistina, alitoa Sakramenti
ya Ubatizo kwa watoto wachanga ishirini, kielelezo cha kazi ya Roho Mtakatifu anayeendelea
kulitajirisha Kanisa kwa watoto wapya wanaozaliwa kwa Maji na Roho Mtakatifu, tayari
kuanza maisha mapya na kuwa ni sehemu ya Jumuiya ya Waamini.
Ubatizo wa Bwana
ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha unyenyekevu wa Kristo katika kutekeleza Mpango
wa Kazi ya Ukombozi, kwa njia ya utii hata kifo cha aibu pale juu Msalabani. Yesu
anaanza maisha yake ya hadhara kwa kupewa Ubatizo wa toba na wongofu wa ndani kutoka
kwa Yohane Mbatizaji. Mtakatifu wa Mungu na ambaye hakuwa na doa la dhambi, anaonesha
mshikamano wa dhati na wadhambi, ili kutambua umuhimu wa kujipatanisha na Mwenyezi
Mungu, kwa kufanya toba na kuchuchumilia wongofu wa ndani, ili kumrudia Mungu kwa
moyo na akili zote.
Yesu anaonesha ukaribu wake kwa mwanadamu, ili kutoa changamoto
ya kuondokana na ubinafsi na dhambi, ili hatimaye, kumpokea na kumkubali Kristo katika
maisha, ili aweze kuwanyanyua na kuwapeleka kwa Baba yake wa mbinguni. Huu ni mshikamano
wa dhati uliomwezesha Kristo kuzama kabisa katika undani wa maisha ya mwanadamu katika
mambo yote, isipokuwa hakuwa na dhambi. Aliuonja udhaifu wa mwili wa mwanadamu, akamwonea
huruma na kukubali kuteseka pamoja naye, ili kumpatia fursa ya kutubu. Kazi ya Ukombozi
iliyokamilishwa na Yesu Kristo kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, inapania
kuganga wale waliopondeka moyo, kuwafariji wagonjwa pamoja na kuwaondolea dhambi zao.
Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anabainisha kwamba, Ubatizo wa Bwana ni kitendo
cha unyenyekevu na upendo mkuu unaoonesha ile furaha ya ndani inayodhihirisha mshikamano
na Fumbo la Utatu Mtakatifu, linaloonesha kwamba, Yesu Kristo ni Masiha, aliyetumwa
na Baba yake wa mbinguni ili kuwakomboa watu wake kutoka katika utumwa wa dhambi na
mauti; kwa njia ya Fumbo la Msalaba, linaloonesha ile nguvu ya Mungu inayomwokoa mwanadamu
kutoka katika lindi la dhambi. Yesu anatekeleza yote haya kama Mchungaji mwema anayeyamimina
maisha yake, ili kuwakirimia waja wake uzima wa milele na hivyo kuwapatanisha na Baba
yake wa Mbinguni. Ni kwa njia ya Ufufuko kutoka katika wafu kwamba, mwanadamu anakombolewa
kutoka katika mauti na ushindi wa Kristo dhidi ya dhambi unaonekana wazi.
Baba
Mtakatifu anasema, watoto waliobatizwa wanaungana na Yesu katika Fumbo la Pasaka,
chemchemi ya maisha mapya, ili kuweza kushiriki katika Ufufuko wake kwa kuzaliwa tena
upya kwa Maji na Roho Mtakatifu, ili kuwa kweli ni watoto wateule wa Mungu wenye uwezo
wa kumwita Mungu, Abba, yaani Baba! Watoto waliobatizwa wameondolewa dhambi ya asili
na sasa ni sehemu ya watoto wa Kanisa, changamoto ya kuishi kwa ukamilifu wito wao
wa kuwa watakatifu, ili hatimaye, waweze kupata uzima wa milele wanaokirimiwa kwa
njia ya Ufufuko wa Kristo.
Baba Mtakatifu anawakumbusha wazazi wa watoto waliobatizwa
kwamba, kwa kuwaombea watoto wao Ubatizo, wanaonesha imani na furaha ya kuwa Wakristo
na mawe hai katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Ni furaha ya
kujitambua kwamba wao kweli ni watoto wa Mungu, wanaokumbatia upendo wa Mungu na ile
furaha ya kuungana na Kristo ndiyo inayowaongoza katika hija ya maisha yao kwani Yeye
ni kiini cha maana ya maisha yao. Ni mwanzo wa maisha ya imani yanayojengeka kwa kumfahamu
na kujenga urafiki wa dhati na Kristo, unaompatia mwanadamu uhuru kamili.
Baba
Mtakatifu anawaambia Wazazi wa Ubatizo kwamba, wanayo dhamana nyeti inayowataka kuwasaidia
wazazi wa watoto waliobatizwa katika malezi, kwa kurithisha kweli za kiimani sanjari
na kutolea ushuhuda wa tunu za Kiinjili, ili kuwajengea watoto hawa nafasi ya kuimarisha
uhusiano wao na Kristo, kwa njia ya mifano bora ya maisha na utekelezaji wa fadhila
za Kikristo katika maisha yao, kwa kusimama kidete pasi ya kulegeza kamba! Baadhi
ya watu ndani ya Jamii wanadhani kwamba, wale wanaoishi imani yao kwa ukamilifu ni
watu waliopitwa na wakati! Hata miongoni mwa Wakristo kuna wale wanaodhani kwamba,
uhusiano wao na Kristo ni kizingiti cha uhuru binafsi. Lakini, jambo hili si kweli!
Mwelekeo
huu ni finyu kwani hautambui uhusiano uliopo na Mwenyezi Mungu katika hija ya imani,
unajionesha katika nguvu ya upendo wa Kristo, unaomwondoa mwanadamu kutoka katika
ubinafsi wake na kuwawezesha kujenga mshikamano wa dhati na Mwenyezi Mungu pamoja
na jirani zao, kwani Mungu ni upendo. Hiki ni kielelezo makini cha imani ya Kikristo
inayojionesha pia katika sura ya mwanadamu na hatima yake.
Maji ya Ubatizo
yaliyobarikiwa kwa Ishala ya Utatu Mtakatifu ni chemchemi ya maisha mapya inayobubujika
kutoka kwa Mwenyezi Mungu anayewajalia uwezo wa kuwa kweli ni watoto wake wapendwa.
Watoto hao kwa njia ya Roho Mtakatifu wamejaliwa fadhila za kimungu; yaani: imani,
matumaini na mapendo. Fadhila hizi hazina budi kurutubishwa kwa Neno la Mungu na Sakramenti
za Kanisa, ili kufikia ukomavu utakaomwezesha mwamini kutolea ushuhuda wao kwa Kristo
na Kanisa lake.
Baba Mtakatifu anahitimisha mahubiri yake kwa kuwaweka watoto
waliobatizwa chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria, ili aweze kuwasindikiza
katika kila hatua ya maisha yao.