2013-01-14 09:22:44

Mchango wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya


Askofu Severine Niwemugizi, Makamu Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, mwishoni wa juma, amewasilisha mapendekezo ya Baraza la Maaskofu Katoliki katika mchakato wa kutoa maoni ya Katiba Mpya ya Tanzania, wakati huu, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inapoendelea kupokea maoini kutoka kwa Makundi. Anasema, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linapinga Mahakama ya Kadhi kuanzishwa na kugharimiwa na Serikali na kwamba, hili ni suala ya waamini wa dini ya Kiislam, wanapaswa wao wenyewe kuianzisha na kuigharimia kwa fedha za waamini wenyewe. Mambo ya kidini si vyema yakaingizwa katika masuala na gharama za Serikali.
Mantiki inayoongoza ukweli huu ni kwamba, dini imekuwepo kabla hata ya Serikali, kumbe, dini inaweza kuongoza mambo yake bila ya kuhitaji ridhaa ya Serikali. Pili, waamini wasiokuwa wa dini ya Kiislam hawaifahamu kwa undani misingi ya Mahakama ya Kadhi, kwani Kadhi ni Mtawala ana Hakimu. Sifa ya kuwa Kadhi ni lazima uwe mwamini wa dini ya Kiislam. Canada ni mfano bora wa kuigwa katika kuendesha Mahakama ya Kadhi.
Akizungumzia kuhusu Tanzania kuwa na uhusiano wa Kidiplomasia na Vatican, Askofu Niwemugizi alifafanua kwamba, tangu Mwaka 1929 katika Mkataba wa Laterano, Vatican ilijitenga na Italia na hivyo kuwa ni nchi huru inayojitegemea kwa mambo yake na kwamba, inatambulikana hivyo hata katika Jumuiya ya Kimataifa na wala si Shirika au Jumuiya ya Kidini. Ikiwa Tanzania inataka kuvunja uhusiano wake wa Kidipolomasia na Vatican iko huru na ni sawa na kuvunja uhusiano na nchi kama Iran.
Askofu Niwemugizi, ambaye kitaaluma ni Jaalim wa Sheria za Kanisa, anafafanua kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limeweka bayana ukweli huu, kutokana na uvumi unaoendelea kuzagaa nchini Tanzania kwamba, Serikali inaoongozwa na kuendeshwa kwa mfumo wa Kanisa Katoliki na shinikizo kutoka kwa Waamini wa dini ya Kiislam kwamba, sasa umefika wakati kwa Tanzania kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislam, OIC. Lakini, ikumbukwe kwamba, lengo la OIC ni kueneza Uislam na kufuta Ukristo katika nchi wanachama. Kumbe, OIC haipaswi kuingizwa katika Katiba, kwa vile Tanzania ina uhusiano wa Kidiplomasia na Vatican.
Kwa uapnde wake Amri mkuu wa Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislam nchini Tanzania, ameitaka Tume ya Marekebisho ya Katiba kutofanyia mzaha suala la Mahakama ya Kadhi na kupendekeza kwamba, suala hili linapaswa kutambulika Kikatiba na kugharimiwa na Serikali. Mahakama ya Kadhi itaongozwa na wasomi wa Sheria za dini ya Kiislam ambao watatoa hukumu kwa masuala ya ndoa, mirathi na talaka.
Anasema, ikiwa kama suala hili litaachiwa mikononi mwa Waislam wenyewe wanaweza kujikuta wakitumia Sharia, kinyume cha Sheria za Nchi. Waamini wa dini ya Kiislam wanataka Ijumaa, iwe ni Siku ya Mapumziko Kitaifa kwa Waislam wote na wanafunzi waruhusiwe kwenda misikitini inapofika saa sita mchana.All the contents on this site are copyrighted ©.