Katiba Mpya ya Tanzania izingatie: haki msingi za binadamu, uhuru wa kuabudu na uhai
wa binadamu dhidi ya utamaduni wa kifo!
Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma, Tanzania anasema kwamba, kwa
miaka kadhaa, watanzania wameonesha hitaji la kuwa na Katiba Mpya, itakayokidhi mahitaji
ya watanzania kwa sasa. Hitaji hili linadai mabadiliko ya kina miongoni mwa viongozi
wa Serikali, viongozi wa vyama vya kisiasa, viongozi wa kidini na wananchi kwa ujumla
wao. Kanisa Katoliki limeendelea kuwa mstari wa mbele kuwahamasisha Wakatoliki kushiriki
kikamilifu katika mchakato wa kutoa maoni yao kuhusu Katiba Mpya ya Tanzania. Mambo ya kuzingatia
kwanza kabisa ni kuhakikisha kwamba, haki msingi za binadamu na uhuru wa watu unaheshimiwa,
sanjari na uhuru wa kidini, ambao ni mhimili wa haki msingi za binadamu. Kwa vile
Katiba ya nchi ni Sheria Mama, kamwe isibebe wala kukumbatia udini unaoweza kuwa ni
shinikizo kutoka kwa makundi ya kidini nchini Tanzania. Sharia, Mahakama ya Kadhi
na Mahakimu wa Makahaka ya Kadhi ni mambo ambayo hayapaswi kuingizwa kwenye Katiba
ya Tanzania, kwani Tanzania kimsingi ni nchi ambayo haina dini na wala Serikali yake
haina dini, lakini watu wake wa dini na imani zao zinazopaswa kuheshimiwa na kulindwa
Kikatiba. Shinikizo kutoka katika makundi ya kidini linaweza kuvuruga misingi ya haki,
amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa. Imani zisipingane na haki msingi za binadamu.
Kama kuna kundi linalotaka uwapo wa Mahakama ya Kadhi, basi ijitegemee na wala isiwe
ni sehemu ya shughuli za Serikali. Kanisa Katoliki lina Mahakama yake, lakini
hiki ni chombo huru kinachojitegemea na hakihitaji ridhaa ya ya Serikali ili kutekeleza
majukumu yake. Katiba Mpya itetee na kulinda maisha ya mtu tangu pale anapotungwa
mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika, kamwe Katiba isikumbatie utamaduni wa kifo.
Kuna haja pia ya kufuta adhabu ya kifo!