Kanisa Katoliki linapania kuendeleza majadiliano ya kidini kwa njia ya ushuhuda wa
maisha!
Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini anasema
kuna haja ya kuendelea kujenga na kuimaraisha utamaduni wa majadiliano ya kidini kuhusu
masuala ya uwepo na umuhimu wa Mwenyezi Mungu katika maisha ya watu, kutokana na ukweli
kwamba, watu wengi wanamezwa na malimwengu, kiasi cha kushindwa kutambua uwepo wa
Mungu kati yao. Mwaka 2012 umekuwa
na matukio muhimu sana katika mchakato wa kudumisha majadiliano ya kidini kati ya
Wakristo na Waamini wa Dini ya Kiislam, mintarafu Mwongozo wa Baraza hili kama unavyobainishwa
na Waraka wa Kristo Mchungaji Mwema. Lengo ni kuendeleza majadiliano ya kidini kwa
njia mbali mbali, lakini zaidi katika ushuhuda wa maisha, daima wakitafuta kutambua
na kuimarisha tunu msingi za maisha ya kiroho, hasa wakati huu watu wanapoonesha kiu
ya kutaka kumfahamu Mungu kwa undani zaidi. Majadiliano ya kidini na Waamini wa
Dini ya Kiislam yanaendelea kupewa kipaumbele cha pekee kama njia ya kutaka kujenga
na kudumisha misingi ya haki, amani, usalama na utulivu, daima wakiwa wanatafuta mafao
ya wengi ndani ya Jamii. Sharia ya dini ya Kiislam anasema Kardinali Tauran imekuwa
ni chanzo cha migogoro ya kidini sehemu mbali mbali za dunia na kikwazo cha majadiliano
ya kidini katika nchi kama Pakistan na Nigeria ambako watu wasiokuwa na hatia wanaendelea
kupoteza maisha yao kutokana na chuki na uhasama wa kidini. Kwa bahati mbaya misimamo
mikali ya kiimani inaweza kupelekea watu wengi wakakosa uelewa na maana sahihi na
tunu bora za maisha ya kiroho zinazofumbatwa katika dini ya Kiislam. Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita, wakati wa hija yake ya kichungaji nchini Lebanon kama sehemu
ya kuzindua matunda ya Sinodi ya Maaskofu Katoliki Mashariki ya kati, alibainisha
kwa kina na mapana utashi wa Kanisa Katoliki kuendeleza mchakato wa majadiliano ya
kidini na waamini wa dini ya Kiislam; majadiliano yanayojikita katika heshima na ukweli;
toba, wongofu wa ndani pamoja na dhamana ya Mama Kanisa kutangaza Injili ya Kristo
hadi miisho ya dunia, kama alivyobainisha wakati wa hotuba yake ya matashi na kheri
ya Siku kuu ya Noeli kwa Mwaka 2012. Kanisa Katoliki linaendelea kushirikiana na
waamini wenye mapenzi mema katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini sehemu
mbali mbali za dunia, kama inavyojionesha kwa kuwa ni mwanachama mwanzilishi wa Kituo
cha KImataifa cha Majadiliano ya Kidini na Kitamaduni, kilichofunguliwa mjini Vienna,
hapo tarehe 26 Novemba 2012. Ni kituo muafaka cha majadiliano katika ukweli, uwazi,
heshima na kuthaminiana kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kardinali
Tauran anasema mwaka 2012 umekuwa ni mwaka wenye matukio mbali mbali yanayoonesha
umuhimu wa kuendeleza majadiliano ya kidini, ili kujenga misingi ya haki, amani, upendo
na mshikamano wa dhati; waamini wa dini zote wanapaswa kushirikiana kwa dhati kwa
ajili ya mafao ya wengi, hakuna maendeleo ya kweli pasi na amani. Dini zichangie katika
ujenzi wa haki, amani, upendo na maelewano. Maadhimisho ya Mwaka wa Imani ni fursa
kwa Wakristo kufahamu kwa kina imani yao kuhusu Yesu Kristo Mkombozi wa dunia, kwa
kuwashirikisha wengine ile furaha ya kukutana na Kristo katika maisha na kweli za
Kiinjili. Hata katika umaskini wake, Kanisa linapenda kutoa mwaliko wa pekee kwa Watoto
wake, kutolea ushuhuda makini wa Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; kwa kuwahakikishia
wote wanaowashangaa kwamba, kwa hakika wamekutana na Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliye
hai.